• HABARI MPYA

  Sunday, February 23, 2014

  YANGA SC SASA SAFI, HAITAKUWA AJABU AL AHLY AKIFUNGISHWA VIRAGO

  MABADILIKO makubwa ya kiuchezaji jana yameshuhudiwa katika kikosi cha Yanga SC ikiifunga mabao 7-0 timu ngumu, Ruvu Shooting katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Ushindi huo dhahiri utawatisha wapinzani wao katika Ligi ya Mabingwa Afrika mwezi ujao, Al Ahly ya Misri watakaomenyana nao Jumamosi ijayo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa kwanza Hatua ya 16 Bora.
  Ushindi huo unaifanya Yanga SC irejee kileleni mwa Ligi Kuu baada ya kutimiza pointi 38, mbili zaidi ya Azam inayoangukia nafasi ya pili sasa, ambayo leo inamenyana na Prisons ya Mbeya Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam. 

  Hadi mapumziko, tayari Yanga SC walikuwa mbele kwa mabao 4-0 yaliyotiwa kimiani na Didier Kavumbangu, Simon Msuva, Emmanuel Okwi na Mrisho Ngassa.
  Yanga SC jana ilibadilika mno kiuchezaji na kuonyesha soka ya kiwango cha juu, tofauti na soka yao iliyozoeleka ya bila mipango inayosababisha kupoteza nafasi nyingi.
  Ngassa alicheza nafasi ya kiungo mchezeshaji mbele ya mkabaji Frank Domayo na kuiongoza vyema timu, hata kuwa chachu ya ushindi huo mnono.
  Kavumbangu alifunga dakika ya kwanza kwa shuti kali baada ya kupokea pasi ya Okwi, wakati Msuva alifunga dakika ya pili kwa shuti pia baada ya pasi ya Ngassa. 
  Okwi aliifungia Yanga dakika ya 28 baada ya pasi ya Mrisho Ngassa na kumlamba chenga kipa Abdallah Ramadhani na dakika mbili baadaye, Ngassa akafunga la nne baada ya kumtoka beki Mangasini Mbonosi.
  Kipindi cha pili, Yanga SC ilirudi na moto wake na kupata mabao matatu zaidi. Kavumbangu alifunga bao la tano dakika ya 53 akimalizia krosi ya Msuva.
  Mganda Hamisi Kiiza ‘Diego’ alinogesha karamu ya mabao ya Yanga SC jana kwa kufunga bao la sita dakika ya 69 akimalizia pasi ya Msuva.
  Nyota wa mchezo wa jana, Msuva alihitimisha karamu ya mabao ya Yanga SC kwa kufunga bao la saba dakika ya 78.
  Baada ya mchezo huo, Yanga SC ilirejea kambini Bagamoyo, Pwani kuendelea na maandalizi ya mechi yake ya kwanza ya Hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa dhidi ya Al Ahly Machi 1, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Ushindi mkubwa zaidi kwa Yanga SC katika historia ya Ligi Kuu unabaki kuwa wa mabao 8-0 dhidi ya Kagera Stars (sasa Kagera Sugar) mwaka 1998, siku ambayo Edibily Jonas Lunyamila pekee alifunga mabao matano.   
  Pongezi kwa benchi la Ufundi la Yanga SC chini ya kocha Mkuu, Mholanzi Hans van der Pluijm kwa kazi nzuri iliyoleta soka maridadi jana.
  Jamani, hivyo ndivyo ambayo watu wanataka kuona timu zetu zinazoajiri makocha wa kigeni zinacheza soka ya kuvutia na ya ushindi.
  Mambo machache tu yameonekana kufanyiwa kazi ndani ya Yanga, namna ya kutengeneza nafasi na kuzitumia, kwa ujumla staili fulani ya uchezaji ya kufika kwenye lango la wapinzani mapema zaidi ilionekana Yanga jana.
  Ndiyo maana ndani ya dakika mbili, tayari Yanga ilikuwa inaongoza mabao mawili.
  Ngassa ametuonyesha ana kipaji kiasi gani zaidi ya kukimbia kimbia na mpira pembezoni mwa Uwanja, kwa kucheza vizuri nafasi ya kiungo jana.
  Alikuwa anagawa pasi vizuri na kuipeleka timu mbele kwa haraka- na timu inapopoteza mpira alikuwa anarudi haraka kusaidia ulinzi.
  Wazi jana Ngassa ile kitu inaitwa ‘Ufaza’ aliiuacha kwenye basi la timu na akaingia uwanjani kufanya kazi moja tu.
  Soka waliyocheza Yanga jana inatia matumaini kwamba inaweza kufanya chochote dhidi ya wapinzani wao katika Ligi ya Mabingwa Afrika, maana Ruvu ni kipimo kizuri tu kwani ni timu ambayo siku zote imekuwa ikiisumbua timu hiyo katika Ligi Kuu.
  Bado kuna tatizo kwenye safu ya ulinzi ya Yanga SC, inapitika kwa urahisi mno na ndiyo maana jana Deo Munishi ‘Dida’ aliokoa hatari tatu ambazo angefungwa asingelaumiwa.
  Frank Domayo lazima aangalie sana uchezaji wake, maana wakati mwingine watu wanaweza wakawa wanawatazama Kevin Yondan na Nadir Haroub ‘Cannavaro’, kumbe hata kiungo mkabajaji ni tatizo.
  Yondan na Cannavaro lazima mmoja wao aweze kuruka juu kucheza mipira kwa kichwa- hicho ni kitu cha kufanyia mazoezi tu.
  Katika mechi tatu zilizopita, Yanga SC imeshinda mabao 19 na kufungwa mawili. Nilitafakari sana mabao mawili iliyofungwa na Komorozine mjini Moroni wiki iliyopita na kujiuliza kama Yanga inajiruhusu kufungwa mabao mawili na vibonde hao, mbele ya Al Ahly itakuwaje?
  Lakini jana Yanga SC wametuonyesha wamebadilika mno, tena sana na kama watarudia kucheza vizuri dhidi ya Al Ahly ikiwa ni pamoja na kurekebisha makosa madogo madogo yaliyojitokeza yakiwemo ya safu ya ulinzi, basi wanaweza kuing’oa Al Ahly.
  Jumapili njema. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC SASA SAFI, HAITAKUWA AJABU AL AHLY AKIFUNGISHWA VIRAGO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top