• HABARI MPYA

    Friday, February 21, 2014

    HATIMAYE CAF, UEFA WASAINI LILE DILI AMBALO TANZANIA ITANUFAIKA PIA

    Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
    SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) na Umoja wa Vyama vya Soka Ulaya (UEFA) jana wamesaini Mkataba wa Ushirikiano (MoU) kwa ajili ya maendeleo ya mchezo huo katika mabara yao.
    Kwa mujibu wa taarifa ya CAF iliyotumwa BIN ZUBEIRY leo, mkataba wa awali wa MoU utakwenda hadi Julai 31 mwaka 2016 na utafungua milango ya kuboresha ushirikiano baina ya bodi hizo za soka. 
    Rais wa UEFA, Michael Platini wa pili kulia na Rais wa CAF, Issa Hayatou wa pili kushoto wakati wa kusaini MOU jana. Wengine kulia ni Katibu wa UEFA, Gianni Infatino na kushoto Katibu wa CAF, Hicham El Amrani.

    Hiyo itahusu kubadilishana taarifa, uzoefu na programu za maendeleo ya kitaalamu katika maeneo mbalimbali kama Makocha, Marefa, Soka ya Vijana, Soka ya Wanawake, Uandaaji wa Mashindano, Utawala, Masoko, Vyombo vya Habari na majukumu ya kijamii.
    Rais wa CAF, Issa Hayatou na wa UEFA, Michel Platini, walisaini Mkataba huo kwa niaba ya bodi hizo mbili za soka.
    Hayatou alisema; “Makubaliano haya yatasaidia vyama vya soka wanachama wa CAF na kujenga uwigo mpana wa maendeleo katika maeneo mbalimbali ya soka. CAF itakuwa kama mtu wa kati baina ya UEFA na vyama vya soka kuhakikisha wanapata manufaa wanayoyatarajia.”
    Kwa upande wake, Platini alisema; “UEFA ina furaha sana kushirikiana na CAF kubadilishana mawazo na kuchangia fikra za kuendeleza mchezo. Jitihada hizi ni matokeo ya uamuzi wa jumla wa vyama 54 vya soka wanachama wa UEFA, tangu CAF imekuwa mdau mkubwa wa soka duniani.”
    Walioshiriki zoezi la utiwaji saini Mkataba huo ni pamoja na Hicham El Amrani, Katibu Mkuu wa CAF, Gianni Infantino, Katibu Mkuu wa UEFA na Wajumbe wa Kamati Kuu ya CAF.
    Wazi mradi huu utazinufaisha nchi zilizo nyuma zaidi kisoka kama za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, zikiwemo Tanzania, Somalia, Kenya, Uganda, Sudan zote, Ethiopia, Rwanda, Burundi, Eritrea, Djibouti na Zanzibar.

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HATIMAYE CAF, UEFA WASAINI LILE DILI AMBALO TANZANIA ITANUFAIKA PIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top