• HABARI MPYA

  Jumatano, Februari 19, 2014

  MZANZIBARI AOMBEWA ITC ACHEZE UJERUMANI, WENGINE WATATU CHUONI KUUZWA ZIMBABWE

  Na Ameir Khalid, Zanzibar
  WANASOKA watatu wa Zanzibar, akiwemo Said Ali Nassor aliyekuwa akiichezea klabu ya FC Turkey, ni miongoni mwa wanasoka watatu wa Tanzania wanaoombewa hati za uhamisho wa kimataifa (ITC) kwenda kucheza soka nje ya nchi.
  Nassor pamoja na Samuel Chuonyo, wameombewa ITC kwa ajili ya kujiunga na klabu ya VfB Eichastatt ya Ujerumani, na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linafanyia kazi maombi hayo.
  Kikosi cha Chuoni ambacho wachezaji wake watatu wanatakiwa Zimbabwe

  Klabu hiyo ilipanda daraja mwaka 2012 hadi Bayernliga, ambayo ni sawa na daraja la tano katika mfumo wa soka wa Ujerumani.
  Katika hatua nyingine, timu ya Howmine ya Zibambwe imevutiwa na wachezaji watatu wa Chuoni SC na tayari imefanya mazungumzo na uongozi wa klabu hiyo kwa ajili ya kuwasajili msimu ujao.
  Taarifa zinasema kuwa, Howmine iliridhishwa na viwango vya wanandinga hao tangu katika mechi ya kwanza ya mzunguko wa awali Kombe la Shirikisho Afrika uliochezwa mjini Harare Febuari 8, mwaka huu.
  Kocha wa Chuoni Ali Bakari Mngazija, amethibitisha taarifa hizo na kusema pande hizo mbili zilianza mazungumzo tangu nchini Zimbabwe ambayo wamekubaliana baadhi ya mambo ili kuwaruhusu nyota hao wakaitangaze Zanzibar nchini humo.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY leo, Mngazija aliwataja wachezaji hao kuwa ni mshambuliaji Hamadi Mshamata, kiungo George Thomas na mlinzi Saleh Hamad, ambao alisema katika mechi zote mbili Zanzibar na Harare walionesha kiwango kizuri kilichowakosha viongozi wa matajiri hao wa almasi.
  Alifahamisha kuwa, baada ya mazungumzo ya mwanzo nchini Zimbabwe, uongozi wa Chuoni ulisema hauna pingamizi kukubali ofa hiyo ya wachezaji hao kufanya majiribio Zimbabwe, lakini wametaka hatua hiyo ifanyike baada ya kumalizika ligi kuu ya Zanzibar.
  “Soka ni ajira kwa vijana, kwa hivyo hatuna pingamizi kwani huko wanakwenda kukuza viwango vyao, kufanya kazi na kuitangaza nchi yetu kimataifa. Tutafuata taratibu zote za uhamisho ili waende,” alisema Mngazija.
  Hata hivyo, alisema wakati mawasiliano kati ya timu hizo yanaendelea, uongozi wa Howmine umeahidi kutuma tiketi za safari kwa wachezaji hao baada ya kukamilika kwa mazungumzo yao.
  Kama mpango huo utafanikiwa, wachezaji hao wataungana na wengine kadhaa kutoka Zanzibar kucheza soka la kulipwa nje ya nchi, akiwemo Ali Badru ambaye alisajiliwa na Al Canal inayocheza ligi kuu Misri (sasa Simba SC), na Abdi Kassim ‘Babi’ anayecheza soka ligi kuu ya Malaysia.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MZANZIBARI AOMBEWA ITC ACHEZE UJERUMANI, WENGINE WATATU CHUONI KUUZWA ZIMBABWE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top