• HABARI MPYA

  Tuesday, February 18, 2014

  UEFA NA CAF WASAINI BONGE LA DILI AMBALO TANZANIA NA ZANZIBAR ZITANUFAIKA

  Na Prince Akbar, Dar es Salaam
  SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) na Umoja wa Vyama vya Soka Ulaya (UEFA) Alhamisi ya Februari 20, mwaka huu watasaini Mkataba wa Makubaliano  utakaojulikana kama (MoU), makao makuu ya CAF mjini Cairo, Misri.
  Kwa mujibu wa taarifa ya CAF iliyotumwa BIN ZUBEIRY jana jioni, Rais wa CAF, Issa Hayatou na Rais wa UEFA, Michel Platini, watasaini MoU ya ushirikiano wa kuendeleza soka Afrika na Ulaya baina ya mabara hayo mawili. 

  Marais hao wawili watasaidiwa na Hicham El Amrani, Katibu Mkuu wa CAF na Gianni Infantino, Katibu Mkuu wa UEFA. Zoezi hilo litahudhuriwa pia na Wajumbe wa Kamati Kuu ya CAF.
  Mkataba wa awali wa MoU utadumu hadi Julai 31, mwaka 2015 na utafungua milango ya kuboresha ushirikiano baina ya bodi hizo za soka. 
  Hiyo itahusu kubadilishana taarifa, uzoefu na programu za maendeleo ya kitaalamu katika maeneo mbalimbali kama Makocha, Marefa, Soka ya Vijana, Soka ya Wanawake, Uandaaji wa Mashindano, Utawala, Masoko, Vyombo vya Habari na majukumu ya kijamii.
  Kutakuwa na Mkutano na Waandishi wa Habari utakaoongozwa na Marais hao wa CAF na UEFA baada ya kusaini mkataba huo wa MoU saa 5:00 asubuhi kwa saa za Cairo keshokutwa.
  Wazi mradi huu utazinufaisha nchi zilizo nyuma zaidi kisoka kama za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, zikiwemo Tanzania, Somalia, Kenya, Uganda, Sudan zote, Ethiopia, Rwanda, Burundi, Eritrea, Djibouti na Zanzibar.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: UEFA NA CAF WASAINI BONGE LA DILI AMBALO TANZANIA NA ZANZIBAR ZITANUFAIKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top