• HABARI MPYA

  Tuesday, February 25, 2014

  NYOTA SITA YANGA WACHOMOLEWA KAMBINI WAKAITUMIKIE STARS...NI PIGO MAANDALIZI DHIDI NYA AL AHLY

  Na Waandishi Wetu, Dar es Salaam
  SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limetangaza kikosi cha wachezaji 22 kwa ajili ya mechi ya kirafiki ya kalenda ya FIFA dhidi ya Namibia (Brave Warriors) itakayochezwa Machi 5 mwaka huu jijini Windhoek, Namibia, ndani yake wakiwemo wachezaji sita wa Yanga SC.
  Hao ni kipa Deogratius Munishi ‘Dida’, beki Kevin Yondan, viungo Athuman Idd, David Luhende, Frank Domayo na Mrisho Ngassa. 
  Kikosi cha kwanza cha Yanga SC ambacho wachezaji wake wanane watakwenda kutumikia timu zao za taifa

  Tayari wachezaji wengine wawili wa Yanga kutoka Uganda, wameitwa kwenye timu yao ya soka ya taifa, The Cranes kwa ajili ya mchezo dhidi ya Zambia mjini Ndola Machi 5, hao ni Emmanuel Okwi na Hamisi Kiiza.
  Ikumbukwe Yanga SC itacheza mechi ya marudiano na Al Ahly ya Misri mjini Cairo kati ya Machi 7 na 9 katika Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya mchezo wa kwanza Dar es Salaam Machi 1, mwaka huu.
  Kwa nyota hao nane kuitwa timu za taifa za Uganda na Tanzania dhahiri itaathiri maandalizi ya Yanga kwa ajili ya mchezo wa marudiano na Ahly, kwani Okwi na Kiiza watalazimika kwenda Uganda mara tu baada ya mechi ya kwanza na mabingwa hao wa Afrika na kwa kuwa watacheza mechi Ndola Machi 5, maana yake wanaweza kuondoka huko Machi 6 wakati tayari mabingwa wa Bara wakiwa Cairo.
  Na sita wa Stars wataingia kambini timu ya taifa baada ya mechi ya kwanza na Ahly na Machi 3 watasafiri kwenda Namibia na kucheza mechi Machi 5, hivyo kuondoka nchini humo siku inayofuata- maana yake nyota wote nane hawatapata fursa ya kushiriki mazoezi ya Yanga kujiandaa na mchezo wa marudiano na Ahly.
  Hali itakuwa mbaya zaidi kwa Yanga iwapo na Rwanda itawaita Mbuyu Twite na Haruna Niyonzima kwa ajili ya mechi za wiki ijayo za kalenda ya FIFA.  
  Kikosi kamili cha Stars kilichotajwa leo ni makipa Deogratius Munishi (Yanga), Ivo Mapunda (Simba) na Mwadini Ally (Azam). Mabeki wa pembeni ni Edward Charles (JKT Ruvu), Erasto Nyoni (Azam), Hassan Mwasapili (Mbeya City) na Michael Aidan (Ruvu Shooting).
  Mabeki wa kati ni Aggrey Morris (Azam) na Kelvin Yondani (Yanga) wakati viungo ni Amri Kiemba (Simba), Athuman Idd (Yanga), David Luhende (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Jonas Mkude (Simba) na Mwinyi Kazimoto (Markhiya Sports Club, Qatar).
  Washambuliaji ni Athanas Mdamu (Alliance Mwanza), Haruna Chanongo (Simba), Khamis Mcha (Azam), Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Mrisho Ngasa (Yanga), Ramadhan Singano (Simba) na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC).
  Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itaingia kambini Machi 1 mwaka huu, kwenye hoteli ya Accommondia inatarajiwa kuondoka Machi 3 mwaka huu kwenda Windhoek.
  TFF imesema wachezaji ambao timu zao zinacheza mechi za mashindano ya kimataifa na ligi wikiendi hii wataripoti kambini mara baada ya mechi zao kumalizika.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NYOTA SITA YANGA WACHOMOLEWA KAMBINI WAKAITUMIKIE STARS...NI PIGO MAANDALIZI DHIDI NYA AL AHLY Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top