• HABARI MPYA

  Jumanne, Februari 25, 2014

  YANGA SC WAINGIA KAMBINI BAHARI BEACH HOTEL, MAZOEZI BOKO

  Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
  KIKOSI cha Yanga SC kinaingia kambini muda huu katika hoteli ya Bahari Beach, Dar es Salaam baada ya kumaliza kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Boko.
  Yanga imefuta mpango wa kurejea Bagamoyo kuweka kambi kwa ajili ya mchezo wake wa Jumamosi dhidi ya mabingwa wa Afrika, Al Ahly au National ya Misri na sasa itabaki Dar es Salaam.
  Kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm amesema Uwanja waliokuwa wanafanyia mazoezi Bagamoyo haufai kwa maandalizi ya mechi hiyo ya kwanza, Hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika anahitaji Uwanja mzuri ambao Bagamoyo haupo kabisa.
  Vyumba vya hoteli ya Bahai Beach na chini ni mwonekano wa ndani
  Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Kimataifa ya Yanga SC, Seif Ahmed ‘Magari’ tangu jana alikuwa ‘bize’ na kutafuta Uwanja mzuri na kambi nzuri na hatimaye jithada zimezaa matunda.
  Yanga SC itamenyana na Ahly Jumamosi ikiwa katika kiwango kizuri kimchezo, imeweza kushinda mabao 19 ndani ya mechi tatu, 14 katika mechi mbili mfululizo za nyumbani 7-0 dhidi ya Komorozine ya Comoro hatua ya Awali ya Ligi ya Mabingwa na 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting katika Ligi Kuu Jumamosi.
  Yanga SC ambayo iliifunga 5-2 Komorozine kwenye mchezo wa marudiano Moroni, katika mechi na Ruvu ilionyesha soka ya kiwango cha juu ambayo imeibua matumaini kwamba inaweza kufurukuta mbele ya Ahly.     
  Mara ya mwisho Ahly iliifunga CS Sfaxien katika mchezo wa Super Cup ya Afrika, lakini haina rekodi ya kuvutia sana kwenye ligi ya Misri msimu huu.
  Ahly inatarajiwa kutua Dar es Salaam kuanzia leo na haitahitaji msaada wa Yanga kwa sababu mapema mwezi huu ilituma wawakilishi wake kushughulikia masuala ya kambi na Uwanja wa mazoezi.
  Hoteli ipo ufukweni mwa Bahari ya Hindi na ina bwawa zuri la kuogelea na gym ya mazoezi ya viungo

  Waarabu hao wanaweza kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Gymkhana, uliopo kando ya bahari ya Hindi na wapi wataweka kambi, haijajulikana ila inaweza kuwa kwenye moja ya hoteli za nyota tano Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA SC WAINGIA KAMBINI BAHARI BEACH HOTEL, MAZOEZI BOKO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top