• HABARI MPYA

  Sunday, November 12, 2017

  MBAO WANAAMINI WATAZINDUKA NA KUDHIHIRISHA UBORA WAO LIGI KUU

  Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
  MWENYEKITI wa Mbao FC, Solly Zephania Njashi amesema kwamba anaamini timu yake itazinduka na kufanya vizuri katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo kwa simu kutoka Bunda ambako amekwenda kwenye msiba, Njashi amesema kwamba baada ya mwanzo usioridhisha timu itasimama imara.
  “Kama utaona, sisi tumeanza na mechi ngumu ngumu kidogo na zile nyepesi zimekuwa za ugenini, ambako mara nyingi hakuna uchezeshaji wa haki. Wewe subiri tu muda si mrefu tutaanza kushinda mfululizo,”amesema Njashi.
  Amesema ni mapema mno kuanza kuitabiria Mbao FC kushuka Daraja wakati Ligi Kuu haijamaliza hata mzunguko wa kwanza.
  “Ligi bado sana hii, msimu uliopita pia baada ya mzunguko wa kwanza Mbao FC ilikuwa miongoni mwa timu zilizokuwa zinatabiriwa kushuka, lakini tumebaki. Nataka nikuthibitishie, tutazinduka hivi karibuni na kuanza kushinda,”amesema Njashi.
  Kwa sasa, washindi hao wa pili wa Azam Sports Federation Cup wanashika nafasi ya 10 katika msimamo wa Ligi Kuu ya timu 16, ikiwa na pointi nane baada ya kucheza mechi tisa, ikiizidi kwa pointi tatu tu Ruvu Shooting inayoshika mkia.
  Timu hiyo iliyo katika Ligi Kuu kwa msimu wake wa pili, itashuka tena dimbani Novemba 18 katika mchezo mwingine wa ugenini dhidi ya wenyeji, Maji Maji Uwanja wa Maji Maji mjini Songea. 
  Na katika kujiandaa na mchezo huo, leo Mbao FC itacheza mechi ya kirafiki na Njombe Mji FC Uwanja wa Amani, Makambako.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MBAO WANAAMINI WATAZINDUKA NA KUDHIHIRISHA UBORA WAO LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top