• HABARI MPYA

  Sunday, January 07, 2024

  SALAH AFUNGA AASISTI, MISRI YAICHAPA TANZANIA 2-0 CAIRO


  WENYEJI, Misri wameibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Tanzania usiku huu Uwanja wa Cairo international Jijini Cairo katika mchezo wa kirafiki timu hizo kujiandaa na Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
  Mabao ya Misri, mabingwa mara saba (1957, 1959, 1986, 1998, 2006, 2008 na 2010) yamefungwa na kiungo Trabzonspor ya Uturuki, wa Mahmoud Ahmed Ibrahim Hassan ‘Trézéguet’ dakika ya 32 na mshambuliaji wa Liverpool, Mohamed Salah Hamed Mahrous Ghaly kwa penalti dakika ya 73.
  Salah ndiye aliyetoa na pasi ya bao la kwanza la Misri, wakati Nahodha wa Tanzania, mshambuliaji wa PAOK ya Ugiriki, Mbwana Ally Samatta alishindwa kuendelea na mchezo baada ya kuumia dakika ya 52 nafasi yake kuchukuliwa na mshambuliaji wa Simba SC ya nyumbani, Kibu Denis Prosper.
  Taifa Stars na Misri zote zinaondoka kesho kwenda Ivory Coast kwa ajili ya Fainali za Kombe la Mataifa y Afrika zinazotarajiwa kuanza Januari 13 hadi Februari 11.
  Misri imepangwa Kundi B pamoja na Ghana, Cape Verde na Msumbiji, wakati Tanzania ipo Kundi F dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Morocco na Zambia.
  Taifa Stars itacheza mechi yake ya kwanza na Morocco Januari 17, kabla ya kukipiga na Zambia Januari 21 Uwanja wa Laurent Pokou Jijini San-Pédro na kumaliza na DRC Januari 24 Uwanja wa Amadou Gon Coulibaly mjini Korhogo.
  Kwa upande wao Mafarao wataanza na Msumbiji Januari 14, kabla ya kucheza na Ghana Januari 18 na kumalizia na Cape Verde Januari 22 mechi zote Uwanja wa Felix Houphouet Boigny Jijini Abidjan. 
  Kwa Taifa Stars hizi ni Fainali za Tatu za Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya mwaka 1980 nchini Nigeria na mwaka 2019 hapa Misri, wakati Mafarao wanakwenda kwenye Fainali za 26.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SALAH AFUNGA AASISTI, MISRI YAICHAPA TANZANIA 2-0 CAIRO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top