• HABARI MPYA

  Sunday, January 21, 2024

  MSUVA AFUNGA STARS YADROO NA ZAMBIA WACHACHE


  TIMU ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Zambia katika mchezo wa Kundi F Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) leo Uwanja wa Laurent Pokou Jijini San-Pedro nchini Ivory Coast.
  Taifa Stars iliuanza vyema mchezo huo na Kufanikiwa kupata bao la kuongoza dakika ya 11 tu kupitia kwa mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Simon Happygod Msuva aliyemalizia pasi ya Nahodha na mshambuliaji wa PAOK ya Ugiriki, Mbwana Ally Samatta.
  Zambia ikapata pigo dakika ya 44 baada ya kiungo wake, Roderick Kabwe anayechezea Sekhukhune United ya Afrika Kusini kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 44 kufuatia kuonyeshwa kadi ya pili ya njano.
  Bado Chipolopolo wakamudu kusawazisha bao hilo kupitia kwa mshambuliaji wa Leicester City, Patson Daka dakika ya 88 akimalizia kwa kichwa kona ya kiungo wa Simba ya Tanzania, Clatous Chama.
  Mechi nyingine ya Kundi F leo, Morocco pia ilitoa sare ya kufungana bao 1-1 na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) hapo hapo Uwanja wa Laurent Pokou.
  Morocco walitangulia kwa bao la beki wa PSG ya Ufaransa, Achraf Hakimi dakika ya sita akimalizia pasi ya kiungo wa Galatasaray ya Uturuki, Hakim Ziyech, kabla ya mshambuliaji wa Stuttgart ya Ujerumani, Silas Katompa Mvumpa kuisawazishia DRC dakika ya 76 akimalizia pasi ya mshambuliaji wa Young Boys ya Uswisi, Meschak Elia.
  Msimamo wa Kundi F sasa ni Morocco pointi nne kileleni, wakifuatiwa na DRC na Zambia zenye pointi mbili kila moja, wakati Tanzania yenye pointi moja inashika mkia kuelekea mechi za mwisho wiki ijayo.
  Taifa Stars itamaliza na DRC, wakati Zambia itamaliza na Morocco.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MSUVA AFUNGA STARS YADROO NA ZAMBIA WACHACHE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top