• HABARI MPYA

    Wednesday, January 17, 2024

    NYOTA WA YANGA, DIARA NA AZIZ KI WAANZA NA SHANGWE AFCON


    NYOTA wa Yanga, kipa Djigui Diarra na kiungo Stephane Aziz Ki jana walianza vyema Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zinazoendelea nchini Ivory Coast baada ya timu zao kushinda mechi za kwanza za makundi yake.
    Aziz Ki alicheza kwa dakika 86 kabla ya kumpisha mshambuliaji wa Amiens SC ya Ligue2 Ufaransa, Boureima Hassane Bandé Burkina Faso ikishinda 1-0 dhidi ya Mauritania katika mchezo wa Kundi D Uwanja wa Bouake.
    Bao pekee la Burkina Faso lilfungwa kwa mkwaju wa penalti na mshambuliaji wa Aston Villa ya England, Bertrand Isidore Traoré dakika ya sita ya muda wa nyongeza baada ya timu dakika 90 za kawaida za mchezo.
    Kwa upande wake, kipa Diarra alikuwa langoni mwanzo hadi mwisho wa mchezo wa Kundi E, akiiongoza Mali kushinda 2-0 dhidi ya Afrika Kusini Amadou Gon Coulibaly mjini Korhogo.
    Mabao ya Mali yalifungwa na beki wa  Real Sociedad ya Hispania, Hamari Traoré dakika ya 60 na mshambuliaji wa Auxerre, Lassine Fanta Mady Sinayoko dakika ya 66.
    Mapema dakika ya 19 mshambuliaji wa Al Ahly ya Misri alipiga juu mkwaju wa penalti na kuikosesha Bafana Bafana nafasi ya bao la kuongoza.
    Mechi nyingine ya Kundi E jana, bao pekee la mshambuliaji wa Orlando Pirates ya Afrika Kusini, Deon Hotto Kavendji dakika ya 88 liliipa Namibia ushindi wa 1-0 dhidi ya Tunisia Uwanja wa Amadou Gon Coulibaly mjini Korhogo.
    Mali sasa inaongoza Kund E kwa wastani wa mabao dhidi ya Namibia, wakifuatiwa na Tunisia ambao wanaizidi wa mabao Afrika Kusini.
    Burkina Faso inaongoza Kundi D ikifuatiwa na Algeria na Angola zenye pointi moja kila moja, wakati Mauritania inashika mkia.
    Mechi za kwanza za makundi zinakamilishwa leo kwa michezo miwili ya Kundi F, Morocco na Tanzania Saa 2:00 usiku na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) dhidi ya Zambia Saa 5:00 usiku Uwanja wa Laurent Pokou Jijini San-Pedro.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NYOTA WA YANGA, DIARA NA AZIZ KI WAANZA NA SHANGWE AFCON Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top