• HABARI MPYA

  Ijumaa, Agosti 14, 2020

  YANGA SC YASOGEZA MBELE UZINDUZI WA WIKI YA WANANCHI KUPISHA SHUGHULI YA KISERIKALI DODOMA KESHO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KLABU ya Yanga SC imessogeza mbele shughuli ya uzinduzi wa Wiki ya Mwananchi iliyokuwa ifanyike kesho Dodoma – kupisha shughuli ya Kiserikali na sasa itafanyika Agosti 22, Jumamosi ya wiki ijayo huko huko Dodoma.
  Kamati ya Habari na Hamasa baada ya kupokea maoni kutoka kwa wanachama, mashabiki, wapenzi, na wadhamini mbalimbali ambao kwa namna moja au nyingine nao wangependa kuwa sehemu ya uzinduzi wa msimu wa Wiki ya Mwananchi 2020 umependekeza uzinduzi huu usogee mbele kwa wiki moja zaidi.
  "Hii ni mara ya kwanza msimu wa Wiki ya Mwananchi kuwa na uzinduzi maalumu ndani ya mikoa ya Tanzania Bara, kufuatia uzinduzi kama huu wa Wiki ya Mwananchi 2019 uliofanyika Visiwani Zanzibar kwa mafanikio makubwa. Kuanzia na uzinduzi Dodoma, makao makuu ya nchi, pia kumeleta hamasa kubwa kwa wadau ambao kila mmoja anataka kuwa sehemu ya historia nyingine kwenye safari ya Timu ya Wananchi", amesema Mwenyekiti wa Kamati ya Habari na Hamasa, Suma Mwaitenda.
  Kamati ikishirikiana na wanachama wa Yanga waliopo Dodoma kama waratibu wenza, wataitumia hii wiki moja ya nyongeza kuweka sawa mahitaji yote ya wadau walioomba kushiriki kwenye uzinduzi wa Wiki ya Mwananchi 2020.
  Kusogezwa mbele kwa wiki moja pia kunawapa fursa wakazi wa mikoa ya jirani na Dodoma kuweza kushiriki kwenye uzinduzi huu unaotarajiwa kuwa wa kipekee.
  Wakati huo huo: Hafidh Saleh amerejeshwa kwenye wadhifa wa Umeneja Yanga SC baada ya miezi 10 tangu alipoondolewa Novemba 5, 2019, wakati ambapo uongozi ulivunja benchi lote la Ufundi.
  "Hafidh ni mzoefu katika eneo hili, amehudumu katika nafasi hiyo kwa kipindi kirefu, hivyo tunaamini katika uwezo na uzoefu wake katika kuihudumia Yanga," amesema Hassan Bumbuli, Afisa Habari.
  Hafidh anatakiwa kuanza kazi mara moja. Uongozi unampongeza kwa jinsi alivyoamua kujitolea katika siku mbili ambazo alikuwa anawasaidia makocha waliopo katika masuala kadhaa kwa ajili ya maandilizi ya timu kwa msimu ujao
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA SC YASOGEZA MBELE UZINDUZI WA WIKI YA WANANCHI KUPISHA SHUGHULI YA KISERIKALI DODOMA KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top