• HABARI MPYA

  Ijumaa, Agosti 21, 2020

  MO’ DEWJI ASEMA HAJATOA SH. BILIONI 20 SIMBA SC KWA SABABU MFUMO WA MABADILIKO HAUJAKAMILIKA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba SC, Mohamed ‘Mo’ Dewji amesema kwamba mfumo wa mabadiliko bado haujakamilika hivyo si wakati mwafaka kuzungumzia uwekezaji wake wa Sh. Bilioni 20 katika klabu hiyo. 
  Akizungumza na Waandishi wa Habari leo katika ofisi za kampuni ya Mohamed Enterprises Limited (MeTL), jengo la Golden Jubilee Tower Jijini Dar es Salaam, Mo Dewji amesema kwamba mfumo utakapokamilika kila kitu kitakwenda sawa.
  “Bilioni 20 zipo, kwa sasa kila mwaka natoa bilioni 3 kama ruzuku kwa klabu. Naamini asilimia kubwa ya Wanasimba wananielewa, kama hunielewi, basi,”amesema.
  “Kwa sasa tupo vizuri. Mungu atutangulie, kesho ni Simba Day. Niwashukuru sana mashabiki sababu bila wao tusingekuwa hapa. Kauli yetu ya Nguvu Moja ipo pale pale na kesho tujitokeze kwa wingi,” ameongeza.
  Dewji amesema kwamba haridhishwi na kushinda tu ubingwa wa ndani, bali malengo yake ni kuiwezesha Simba SC kutwaa hadi ubingwa wa Afrika.
  “Malengo yetu sasa ni kuendelea kushindana ndani na kushinda ubingwa, lakini pia kufika kwenye hatua ya makundi ya Ligi ha Mabingwa Afrika. Mipango yetu mwaka huu ni kujenga hosteli za timu, uwekezaji wa GPS ambao tutakuwa tunaona takwimu za wachezaji,” amesema.
  Aidha, Mo Dewji amesema kwamba hivi karibu watatangaza nafasi za kazi zaidi na mojawapo itakuwa ya Mkurugenzi wa Ufundi.
  “Tutaanzisha akademi, kutakuwa na watu ambao watazunguka nchini kutafuta vipaji. Ambao watachaguliwa tutawaleta Dar na tutamgharamia. Tutakuza kipaji chake na tutamlipia gharama za shule,”ameongeza.

  Kikosi cha Simba SC kesho kitateremka Uwanja wa Mkapa kumenyana na Vital’O ya Burundi katika mchezo wa kirafiki kwenye tamasha la Simba Day, ambalo msanii Nassib Abdul ‘Diamond Platnmuz’ atatumbuiza.
  Na kuelekea kwenye mchezo huo, kocha mkuu wa Simba SC, Mbelgiji Sven-Ludwig Vandenbroeck amesema; “Mchezo wa kesho ni wa kufurahia kwa mashabiki, inatakiwa kuwa siku ya kufurahi. Wachezaji wetu waliokuwepo na wapya watatambulishwa wote,”.
  Kikosi cha Simba leo kimefanya mazoezi yake Uwanja wa Mkapa, yakiwa ni maandalizi ya mwisho kabla ya mchezo dhidi ya Vital’O kesho.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MO’ DEWJI ASEMA HAJATOA SH. BILIONI 20 SIMBA SC KWA SABABU MFUMO WA MABADILIKO HAUJAKAMILIKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top