• HABARI MPYA

  Jumapili, Agosti 30, 2020

  MORRISON ASETI LA KWANZA, APIGA LA PILI SIMBA YAICHAPA NAMUNGO 2-0 NA KUTWAA NGAO YA JAMII YA SITA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MABINGWA wa mataji yote nchini, Simba SC wamefanikiwa kutwaa na Ngao ya Jamii baaa ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Namungo FC jioni ya leo Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha.
  Nyota wa mchezo wa leo amekuwa ni mchezaji mpya, winga Mghana Bernard Morrison aliyeseti bao la kwanza kipindi cha kwanza na kufunga la pili kipindi cha pili.
  Nahodha John Raphael Bocco aliifungia Simba SC bao la kwanza kwa penalti dakika ya saba baada ya Morrison kuangushwa kwenye boksi – kabla ya winga huyo Mghana kufunga la pili dakika ya 60 akimalizia pasi ya kiungo Mzambia, Clatous Chama.  Na huo unakuwa ushindi wa sita wa Ngao ya Jamii kwa Simba SC tangu ianzishwe mwaka 2001, na kuwa timu iliyobeba taji hilo mara nyingi zaidi, ikifuatiwa na watani wa jadi, Yanga SC waliotwaa mara tano. 
  Simba SC imebeba Ngao ya Jamii katika miaka ya 2011 ikiifunga Yanga 2-0, 2012 ikiifunga Azam FC 3-2, mwaka 2017 ikiwafunga Yanga kwa penalti 5-4 kufuatia sare ya 0-0, 2018 ikiwafunga Mtibwa Sugar 2-1, mwaka 2019 ikiwafunga Azam FC 4-2 na leo.
  Yanga SC walikuwa washindi wa kwanza wa Ngao ya Jamii mwaka 2001, wakati huo ikiitwa Ngao ya Hisani baada ya kuwafunga Simba 2-1, kabla ya kubeba tena 2010 wakiwafunga tena Simba kwa penalti 3-1 kufuatia sare ya 0-0, 2013 wakiichapa Azam FC 1-0, 2014 wakiitandika Azam FC 3-0 na 2015 wakiifunga Azam FC kwa penalti 8-7 baada ya sare ya 0-0.
  Timu nyingine zilizotwaa Ngao ya Jamii ni Mtibwa Sugar mwaka 2009 wakiifunga Yanga SC  1-0 na Azam FC 2016 wakiifunga Yanga pia kwa penalti 4-1 baada ya sare ya 2-2.

  Baada ya mchezo huo, kiungo Jonas Mkude alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mchezo huo na kuzawadiwa fedha taslimu Sh. 500,000.
  Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Joash Onyango, Kennedy Juma, Jonas Mkude, Hassan Dilunga/David Kameta dk78, Muzamil Yassin, John Bocco/Meddie Kagere dk78, Clatous Chama/ na Bernard Morrison/Rally Bwalya dk67.
  Namungo FC; Nourdine Balora, Rodgers Gabriel/Haruna Shamte dk63, Jaffar Mohamed, Steven Duah, Hamisi Fakhi/Hamis Khalfan dk3, Abdulhalm Humud/Aman Kyata dk, Abeid Athumani/Bigirimana Blaise dk46, Lucas Kikoti, Steven Sey, Nzigamasabo Steve na Sixtus Sabilo/Shiza Kichuya dk46.


  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MORRISON ASETI LA KWANZA, APIGA LA PILI SIMBA YAICHAPA NAMUNGO 2-0 NA KUTWAA NGAO YA JAMII YA SITA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top