• HABARI MPYA

    Wednesday, November 04, 2015

    MBEYA CITY INAPOTAKA KUGEUZWA YA ‘MASTAA WA ZAMANI’, YETU MACHO!

    MARA baada ya kuona picha Mkurugenzi wa kampuni ya Bin Slum Tyres Limited, Nassor Bin Slum anamkabidhi Mwenyekiti wa Mbeya City, Mussa Mapunda basi lenye thamani ya Sh. Milioni 180, nilikwenda kutazama msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Lengo ni kujiridhisha, Mbeya City FC ipo katika nafasi ya ngapi katika msimamo huo, mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ukiwa unaelekea ukingoni.
    Mbeya City FC inashika nafasi ya 11 katika Ligi ya timu 16, baada ya kuvuna pointi tisa kwenye mechi 10 za awali walizocheza hadi sasa, kutokana na sare tatu kushinda mechi mbili na kufungwa mechi tano.

    Baada ya kuona nafasi ya Mbeya City na mwenendo wao katika Ligi Kuu kwa ujumla msimu huu, nikajiuliza basi hilo watalitumia katika mechi za Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao?
    Ukweli ni kwamba mwenendo wa Mbeya City katika Ligi Kuu hadi sasa si mzuri na haitakuwa ajabu wakiipa mkono wa kwaheri Ligi Kuu mwishoni mwa msimu.
    African Sports, Kagera Sugar na JKT Ruvu ndizo timu ambazo zina hali mbaya zaidi, lakini nazo zipo kwenye jitihada za kujiimarisha kuelekea mechi zijazo, hususan za mzunguko wa pili.
    Lakini Mbeya City inazizidi kwa pointi nne Kagera Sugar na JKT Ruvu- unaweza kuona mambo yanaweza kubadilika.
    Ni hii Mbeya City ambayo misimu miwili iliyopita ilipanda Ligi Kuu na moja kwa moja kuwa tishio ikiibua vipaji kadhaa vya wachezaji waliokuwa gumzo ndani ya muda mfupi, akiwemo Deus Kaseke ambaye msimu huu amesajiliwa Yanga SC.
    Mbeya City ilianza kuyumba katika msimu wake wa pili tu Ligi Kuu, baada ya msimu uliopita kuanza vibaya kiasi cha kuvumishwa kwamba imemfukuza aliyekuwa kocha wake, Juma Mwambusi.
    Hata hivyo, Mwambusi alibaki kazini na Mbeya City ikazinduka na kumalizia Ligi vizuri, hatimaye tumeendelea kuwa nayo msimu huu. Mwambusi amehamia Yanga SC mwezi uliopita na sasa Meja mstaafu, Abdul Mingange ndiye kocha wa timu hiyo.
    Najaribu kutazama picha ya Mbeya City ya sasa na ile iliyokuja kwa kishindo Ligi Kuu msimu wa 2013-2014 naona vitu viwili tofauti.
    Mbeya City ya sasa inakuja kusajili wachezaji wa mjini walioachwa katika klabu kubwa kwa sababu mbalimbali, ikiwemo nidhamu na kushuka viwango.
    Kabla ya kufikia kuangalia sababu za kuachwa kwao timu za mjini, lakini kuna tatizo kubwa kwa wachezaji waliofikia kucheza timu kubwa, wanaporudi timu ndogo ni wachache ambao huwajibika ipasavyo.
    Wengi wao hujiona kama wapo sehemu ambayo si sawa yao. Wapo katika timu ambayo hawapati changamoto wanazohitaji na hawana cha kujifunza, matokeo yake huonekana kama wenye dharau hivi.
    Na ni wazi wamekwenda huko kwa sababu mjini hawakupata timu nyingine ya kuwasajili- maana yake hawapo huko kwa utashi wao.
    Mchezaji wa aina hiyo si wa kumtarajia sana acheze kwa maslahi ya timu na hakuna ajabu baadhi yao wamekuwa wakifanya vitendo vya utovu wa nidhamu bila kufikiria wataiathiri vipi timu.
    Kusajili wachezaji wazoefu kuimarisha timu si vibaya, lakini ipo haja ya kuangalia idadi na aina ya mchezaji anayesajiliwa atakuwa na faida gani kwa timu.
    Sina sababu ya kumtaja mchezaji yeyote, lakini Mbeya City wenyewe wanajua aina ya wachezaji waliowasajili msimu huu na waliowaacha.
    Unaweza kusema Mbeya City ilishindwa kushindana na Yanga SC kumbakiza Kaseka, au kumzuia Peter Mwalyanzi asiende Simba SC, lakini imekuwaje Paul Nonga kaenda Mwadui?
    Safu ya ushambuliaji ya Mbeya City msimu huu imewapoteza wakali wake kama Kaseke, Mwalyanzi, Nonga na mkongwe Mwagane Yeya, je badala wao wamesajiliwa akina nani?
    Makipa wote wawili wa Mbeya City, Hannington Kalyesebula na Juma Kaseja ni ‘watu wazima’, hata kama ni kutafuta uzoefu katika timu si kwa usajili wa aina hii.
    Mbeya City wanatakiwa kurudi kwenye msingi waliokuja nao, kusaka vipaji ndani ya Mbeya badala ya kuja kusajili wachezaji ‘walioshindikana’ mjini.
    Watu wanashangaa, Yanga SC imekwenda kumsajili Godfrey Mwashiuya wa Kemondo, Mbeya vijijini huko, wakati Mbeya City wamekuja kusajili ‘mastaa wa zamani’ Dar es Salaam.
    Mwashiuya angekuwa na wakati mzuri sana Mbeya City kuliko Yanga SC, kwa sababu angepata nafasi zaidi ya kucheza na kukomaa haraka.
    Lakini tayari viongozi wa Mbeya City akili zao wamezielekeza kusajili ‘mastaa wa zamani’ waliowika timu za mjini badala ya kusaka vipaji ndani ya Mbeya. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MBEYA CITY INAPOTAKA KUGEUZWA YA ‘MASTAA WA ZAMANI’, YETU MACHO! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top