• HABARI MPYA

    Monday, October 06, 2014

    YANGA SC YAZUIA WACHEZAJI WAKE KUJIUNGA NA STARS, KISA…TFF WAHAHA KUWEKA MAMBO SAWA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KLABU ya Yanga SC ya Dar es Salaam imewazuia wachezaji wake saba kujiunga na kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kilichoingia kambini leo kujiandaa na mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Benin mwishoni mwa wiki.
    Wachezaji wa Yanga SC walioitwa Stars inayofundishwa na kocha Mholanzi, Mart Nooij ni kipa Deogratius Munishi ‘Dida’, mabeki Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani, Charles Edward na mawinga Simon Msuva na Mrisho Ngassa.
    Yanga SC imefikia hatua hiyo kwa sababu wanataka wapewe taarifa rasmi ya maandishi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) juu ya uteuzi wa wachezaji hao Stars.
    Wachezaji wa Yanga SC walioitwa Taifa Stars wamezuiwa na uongozi wao kujiunga na timu hiyo

    Wachezaji wote saba wa Yanga SC wameagizwa kutojiunga na kambi ya Stars hadi uongozi wa klabu utakapowaambia kufanya hivyo. 
    BIN ZUBEIRY imewasiliana na Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa juu ya hilo na akasema; “Sisi tulikwishaandika barua kwa klabu zote, hadi za nje wiki iliyopita kuwaomba wachezaji kwa ajili ya mechi, sasa unaponiambia hivyo, nashangaa. Ngoja niwasiliane na Katibu wa Yanga (Benno Njovu),”.
    Hata hivyo, BIN ZUBEIRY ilipomrudia Mwesigwa baadaye, alisema hakufanikiwa kumpaja Njovu kwenye simu, hivyo ataendelea kulishughulikia suala hilo kuhakikisha wachezaji hao kesho wanaingia kambini.
    Taifa Stars na Benin ‘Squirrels’ zitamenyana Oktoba 12, kuanzia Saa 11:00 jioni, mchezo ambao utatanguliwa na mechi ya kudumisha upendo, amani, udugu na ushirikiano kati ya timu za taasisi za dini ya Kiislamu na Kikristo itakayoanza Saa 9:00 Alasiri.
    Kikosi kamili cha Stars kilichoteuliwa kwa ajili ya mchezo huo ni; ni makipa Deogratias Munishi (Yanga), Aishi Manula (Azam), na Mwadini Ali (Azam).
    Mabeki ni Said Moradi (Azam), Shomari Kapombe (Azam), Oscar Joshua (Yanga), Nadir Haroub (Yanga), Kelvin Yondani (Yanga), Aggrey Morris (Azam), Miraji Adam (Simba), Charles Edward (Yanga) na Emmanuel Simwanda (African Lyon).
    Viungo ni Erasto Nyoni (Azam), Mwinyi Kazimoto (Al Markhiya, Qatar), Amri Kiemba (Simba), Himid Mao (Azam), Salum Abubakar (Azam), Said Ndemla (Simba) na Haruna Chanongo (Simba).
    Washambuliaji ni Khamis Mcha (Azam), Simon Msuva (Yanga), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DR Congo), Mbwana Samata (TP Mazembe, DR Congo), Mrisho Ngasa (Yanga), Mwegane Yeya (Mbeya City), na Juma Liuzio (Zesco, Zambia).
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC YAZUIA WACHEZAJI WAKE KUJIUNGA NA STARS, KISA…TFF WAHAHA KUWEKA MAMBO SAWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top