• HABARI MPYA

  Ijumaa, Oktoba 31, 2014

  YANGA SC NA ‘MAZINGAOMBWE’ YA MIKATABA YA WACHEZAJI, AMBAYO MWISHOWE HUWATOKEA PUANI…SASA WANA ‘KIMEO’ CHA KASEJA

  Na Renatus Mahima, DAR ES SALAAM
  KIPA Juma Kaseja Juma ameweka wazi kwamba ana mpango wa kuvunja mkataba wake na Yanga SC endapo klabu hiyo ya Jangwani haitaendelea kutekeleza matakwa yake kwa kumalizia fedha za usajili wake Sh. Milioni 20 na kumchezesha mara kwa mara kwenye kikosi cha timu hiyo.
  Kupitia kwa Meneja wake, Abdulfatah Salim Saleh, Kaseja ameikumbusha Yanga SC kuhusu kumalizia fedha za usajili wake ambazo kwa mujibu wa makubaliano kati yake na klabu hiyo, alipaswa kulipwa Januari mwaka huu lakini hadi sasa hakuna hata senti tano iliyolipwa.
  BIN ZUBEIRY imeutafuta uongozi wa Yanga SC ar es Salaam ambapo kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Beno Njovu umekataa kumtambua meneja wa Kaseja (Abdulfatah) kwa maelezo kuwa hatambuliki katika Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) huku ukikataa kuzungumzia Sh. milioni 20 ambazo kipa huyo aliyekuwa namba moja nchini.
  Juma Kaseja akimdhibiti kiungo wa Simba SC, Awadh Juma katika mechi ya Nani Mtani Jembe Desemba mwaka jana

  “Swali lako la kwanza (kuhusu kumlipa Kaseja Sh. milioni 20 za usajili) siwezi kulijibu kwa sasa. FIFA tangu 2001 haiwatambui mawakala wa wachezaji. Mawakala hao wanatambuliwa na vyama vya soka vya nchi husika, hivyo mchezaji Juma Kaseja hana wakala anayetambuliwa na taasisi yoyote iwe ni YANGA, TFF au FIFA,” anasema na kuongeza:
  “Suala la kumpanga mchezaji ni maamuzi ya kocha ana si mtu yeyote ndani ya timu.”
  Kaseja alisaini Yanga SC mbele ya Meneja wake, Abdulfatah ambaye leo Njovu anasema hamtambui. Tena zoezi lilifanyika ofisini kwa Abdulfatah, katika hoteli ya Sapphire Court, Kariakoo, Dar es Salaam upande wa Yanga SC wahusika wakiwa Isaac Chanji, Abdallah Bin Kleb na Seif Ahmed ‘Magari’.   
  Kama Yanga SC haitatimiza matakwa ya kimakataba kati yake na Kaseja, ni wazi kwamba klabu hiyo itakuwa hatarini kumpoteza kirahisi kipa huyo kama ilivyompoteza mshambuliaji Mganda Emmanuel Okwi dakika za mwisho kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili msimu huu.
  Yanga SC ilishindwa kutimiza matakwa ya kimkata kati yake na Okwi kwa kutomlipa mishahara na kumalizia fedha za usajili Sh. milioni 50, hivyo kuvunja mkataba huo. Ndivyo itakavyokuwa kwa Kaseja ambaye ameripotiwa kuwaniwa na watani wao wa jadi, Simba ambao wanatamani kumrudisha dirisha dogo ili kuimarisha timu yao.
  Hii si mara ya kwanza Yanga SC kufanya vitendo vinavyoashirikia uzembe na ubabaishaji na kuugharimu kwa kupoteza wachezaji muhimu na kulipa mamilioni ya shilingi.
  Mechi tano kabla ya kumalika kwa msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilipokea amri ya Mahakamu Kuu (Kitengo cha Kazi) kuchukua fedha zote za mgawo wa Yanga kutokana na mapato ya milangoni hadi pale Sh milioni 106 za kuwalipa wachezaji wake wa zamanki beki Mmalawi Wisdom Ndlovu na kipa Stephen Malashi zitakapokamilika.
  Juma Kaseja akisaini Yanga SC ofisini kwa Meneja wake, Abdulfatah. Kushoto ni Bin Kleb na nyuma Abdulfatah
  Seif Magari akimshuhudia Kaseja anasaini

  Yanga SC ilivunja mikataba ya wachezaji hao kinyume cha taratibu, matokeo ambayo yameifanya klabu hiyo kuambulia patupu katika mechi zake tano za mwisho msimu uliopita tangu mechi ya Machi 22 mwaka huu kati yake na Rhino Rangers kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora. 
  Yanga SC ilipata mgawo wa Sh. milioni 9.2 kati ya Sh.milioni 38.655 za mapato ya mechi hiyo iliyomalizika kwa Rhino Ranger kufungwa magoli 3-0.
  Yanga imeendelea kukatwa fungu hilo hadi mechi ya watani wa jadi iliyochezwa Oktoba 25, lilipokamilika. Sh. Milioni 9.221 kati ya Sh.milioni 38.655
  TFF, baada ya amri ya Mahakama Kuu, iliwakumbusha wanachama wake, zikiwamo klabu, kuzingatua mikataba wanayooingia na watendaji wao kwa kufuata taratibu pindi wanapotaka kuivunja.
  Mwaja jana Yanga SC pia iliamuliwa na FIFA kumlipa aliyekuwa kocha wake, Mserbia Kostadin Papic malimbikizo ya mishahara ya dola 12, 300 (zaidi ya Sh. milioni 15) na beki wake wa zamani, Mkenya John Njoroge aliyekiwa akiidai milioni 17. 
  Yanga SC pia imekuwa na kesi dhidi ya waliokuwa watendaji wake; Celestine Mwesigwa aliyekuwa katibu mkuu na Louis Sendeu aliyekuwa msemaji wake. Wawili hao walilazimika kutinga Baraza la Uamuzi na Usuluhishi baada ya klabu hiyo kuwatimua pasipo kuwalipa stahiki zao muda mfupi baada ya timu yao kufungwa 3-0 na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro Septemba 19, 2012.
  Baada ya kipigo hicho, Yanga SC pia ilimtimua aliyekuwa kocha mkuu, Mbelgiji Tom Saintfiet na Meneja wa Timu, Hafidh Saleh, ambaye baadaye ilimrejesha madarakani.
  Kutokana na kile kinachoonekana kama kutokuwa makini na pengine kupuuza juu ya matakwa ya mikataba inayoingia na watendaji wake wakiwamo wachezaji, ni wazi kwamba Yanga SC itaendelea kupoteza watu (mfano wachezaji) muhimu katika maendeleo yake.
  Kutomlipa Kaseja fedha za usajili na kumchezesha mara kwa mara kama walivyokubaliana, ni wazi kwamba kutapelekea kuvunjwa kwa mkataba baina ya pande hizo mbili, hivyo klabu hiyo kukosa huduma za kipa huyo katika michuano ya ndani na nje ya nchi.
  Kocha wa Yanga, Mbrazil Marcio Maximo, kama ilivyokuwa wakati akiinoa Taifa Stars, hampi nafasi Kaseja katika kikosi chake cha kwanza VPL, hata hivyo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA SC NA ‘MAZINGAOMBWE’ YA MIKATABA YA WACHEZAJI, AMBAYO MWISHOWE HUWATOKEA PUANI…SASA WANA ‘KIMEO’ CHA KASEJA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top