• HABARI MPYA

  Ijumaa, Oktoba 24, 2014

  MWAMWAJA AWATANGAZIA HALI YA HATARI SIMBA SC MBEYA, OKWI FITI KUWAVAA PRISONS

  Na Renatus Mahima, MBEYA
  WAKATI kocha wa Tanzania Prisons, David Mwamwaja ametangaza vita katika mechi yao ya kesho dhidi ya Simba, kocha wa wapinzani wao, Patrick Phiri ameendelea kusisitiza timu yake itashinda mechi hiyo.
  Simba, ambayo haijapata ushindi katika mechi 10 zilizopita za Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) tangu ilipoifunga Ruvu Shooting 3-2 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam miezi saba iliyopita, leo ni mgeni wa Prisons kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine mjini hapa katika mechi ya raundi ya tano ya ligi hiyo msimu huu.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY mara tu baada ya kumalizika kwa mazoezi ya timu yake kwenye uwanja huo mjini hapa leo asubuhi, Phiri alisema timu yake iko vizuri na ana matumaini leo inapata ushindi wa kwanza msimu huu.
  Kikosi cha Prisons kitamenyana na Simba SC kesho

  "Prisons ni timu nzuri, mechi itakuwa ngumu wa sababu tuko ugenini," alisema. "Tutapambana kuhakikisha tunatimiza kile tulichokiahidi kuanza kushinda baada ya kupata sare katika mechi zilizopita."
  Akizungumzia kuumia wa mshambuliaji Mganda Emmanuel Okwi, Phiri alisema: "Okwi alipata maumivu ya enka wakati wa mazoezi jana, lakini kama ulivyomuona leo amefanya mazoezi vizuri na timu, nitakapopata taarifa ya mwisho kutoka kwa daktari, nitaamua kama atacheza mechi ya kesho au la."
  Akizungumzia majeraha ya Okwi, Yassin Gembe, daktari wa Simba, alisema mchezaji huyo wa zamani wa SC Villa ya Uganda, Etoile du Sahel ya Tunisia na Yanga, yuko fiti wa ajili ya mechi ya kesho.
  "Okwi alipata maumivu kidogo wakati wa mazoezi ya jana kwenye Uwanja wa Jeshi hapa Mbeya, lakini ninashangaa suala hilo limekuzwa na baadhi ya vyombo vya habari. Kwa sasa yuko vizuri. Kocha ndiye mwenye maamuzi ya kumpanga au kutompanga kesho," aliongeza Gembe.
  Mwamwaja naye amesema mjini hapa kwamba amekiandaa vyema kikosi chake kuhakikisha kinalinda heshima baada ya kupoteza nyumbani 2-1 dhidi ya JKT Ruvu katika mechi iliyopita.
  "Kulikuwa na matatizo kidogo yaliyosababishwa na kipa wetu (Beno Kakolanya) na kutugharimu katika mechi iliyopita. Tumeyafanyia kazi na tuko tayari kusaka pointi tatu dhidi ya Simba," alisema kocha huyo aliyewahi kuinoa Simba 1999 akichukua mikoba ya Mohamed Kajole (marehemu).
  "Tumejiandaa kuwathibitishia wapenzi wa soka kwamba walichokisema Simba ni maneno tu, wanapaswa kushukuru kwa kuambulia sare katika mechi zilizopita, tumejindaa kuhakikisha hawapati hata pointi moja hapa (Mbeya)," aliongeza Mwamwaja.
  Kikosi cha Simba kinachocheza mechi yake ya kwanza nje ya Dar es Salaam leo kitakuwa na wakati mgumu mbele ya winga tegemeo wa Prisons, Hamis Maingo ambaye amekuwa mpishi mzuri wa washambuliaji Jeremia Juma na Omar. 
  Prisons pia inajivunia kuwa na safu ya ulinzi imara inayoongozwa na beki wa kati anayetajwa kuwa 'kiboko ya Amissi Tambwe', Nurdin Chona na beki wa pembeni Salum Kimenya ambaye akicheza kama pacha wa winga Maingo.
  Prisons na Simba zilitoka suluhu kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine mjini hapa katika mechi mzunguko wa pili Februari 9, mwaka huu.
  Simba iliyo nafasi ya tisa ya msimamo wa ligi imeruhusu mabao manne na kufunga manne katika mechi tatu za mwanzo ilizotoka sare kabla ya kutoka suluhu na Yanga wiki iliyopita wakati Prisons iko nafasi ya nane ikiwa na pointi nne pia baada ya kushinda 2-0 dhidi ya Ruvu Shooting kabla ya kupoteza 2-1 dhidi ya Yanga, 2-1 dhidi ya JKT Ruvu na kutoka suluhu dhidi ya vinara wa msimamo, Azam FC.
  Phiri tayari ameshaweka wazi kwamba atawaanzisha kipa 'kinda' Peter Manyika Jr na mfungaji bora wa msimu uliopita, Tambwe ambaye hakumpanga katika mechi iliyopita dhidi ya Yanga. 
  Akidaka kwa mara ya kwanza katia kikosi cha kwanza katika mechi iliyopita dhidi ya Yanga, kipa huyo chaguo la tatu aliweka rekodi ya kuwa kipa pekee wa Simba ambaye hajaruhusu nyavu zake kutikishwa baada ya makipa majeruhi Ivo Mapunda na kipa bora wa msimu uliopita Hussein Sharrif 'Casillas' kufungwa magoli mawili kila mmoja.   
  Mechi nyingine za kesho zinawakutanisha Stand United na Yanga kwenye Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga, Coastal Union watakuwa wageni wa Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba wakati Azam FC ni wenyeji wa JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Azam jijini Dar es Salaam.
  Mgambo Shooting ya Tanga imesafiri hadi kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara kumenyana na timu iliyotimua kocha mkuu na kocha wa makipa, Ndanda FC wakati ‘maafande’ wa Ruvu Shooting walioacha ‘dhahama’ Ndanda FC mwishoni mwa wiki wanawaalika wababe wa Mtibwa Sugar, Timu ya Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Mabatini uliopo Mlandizi, Pwani.
  Mbeya City na Mtibwa Sugar zitahitimisha raundi ya tano zitakapokutana kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine mjini hapa katika mechii pekee ya ligi hiyo kesho.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MWAMWAJA AWATANGAZIA HALI YA HATARI SIMBA SC MBEYA, OKWI FITI KUWAVAA PRISONS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top