• HABARI MPYA

  Jumatatu, Oktoba 27, 2014

  BIN SLUM, COCA COLA WAMEMWAGA MAMILONI, WAKALI WAPYA WAMESAJILIWA, TIMU IMEPOTEZA MAKALI, KUNANI MBEYA CITY?

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MSIMU uliopita, wakicheza Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa mara ya kwanza tangu wapande, walipoteza mchezo mmoja tu nyumbani, tena wa mwisho.
  Mbeya City walifungwa 2-1 kwa taabu na Azam FC walioibuka mabingwa- lakini zaidi ya hapo, ni vigogo Simba SC na Yanga SC walioambulia angalau sare kwa timu hiyo Uwanja wa Sokoine.
  Mbeya City ilikuwa tishio ndani na nje ya Sokoine na soka yake ya nguvu na kasi iliwavutia wengi, wakiamini amepatikana mpinzani mpya wa kweli katika Ligi Kuu.
  Lakini mambo yamebadilika msimu huu, Mbeya City jana walifungwa mechi ya pili mfululizo nyumbani, baada ya kuchapwa 2-0 na Mtibwa Sugar Uwanja wa Sokoine.
  Mbeya City ilifanikiwa kumbakiza Saad Kipanga aliyekuwa anatakiwa na Simba SC

  Wiki iliyopita, Mbeya City walifungwa 1-0 na Azam FC hapo hapo Sokoine na kwa ujumla timu hiyo ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya (MCC) imevuna pointi nne katika mechi nne za nyumbani, ikifungwa mbili, sare moja na kushinda moja.
  Ilianza kwa sare ya bila kufungana na JKT Ruvu kabla ya kushinda 1-0 dhidi ya Coastal Union kwa mbinde, bao la penalti kisha ikafungwa mara mbili, 1-0 na Azam na 2-0 na Mtibwa.
  Timu hiyo iliyomaliza katika nafasi ya tatu msimu uliopita, imecheza mechi moja tu ugenini msimu huu na kutoa sare ya bila kufungana na Ruvu Shooting Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
  Hii maana yake, Mbeya City imeporomoka na kupoteza makali yake ya msimu uliopita, licha ya kuonekana ilijizatiti mno kuelekea msimu huu.
  Imepata wafadhili na wadhamini, Coca Cola na Bins Slum Tyres kupitia betri za RB waliomwaga mamilioni ya fedha.
  Imeongeza nguvu kwa kusajili wakali wengine, akiwemo Themi Felix Buhaja kutoka Kagera Sugar na imefanikiwa kuwazuia nyota wake waliokuwa wanawaniwa na klabu za Dar es Salaam, Mwagane Yeya na Saada Kipanga, lakini mambo si mambo hadi sasa, kuna nini Mbeya City?
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: BIN SLUM, COCA COLA WAMEMWAGA MAMILONI, WAKALI WAPYA WAMESAJILIWA, TIMU IMEPOTEZA MAKALI, KUNANI MBEYA CITY? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top