• HABARI MPYA

    Wednesday, October 22, 2014

    YANGA YA MANJI, KULIPA 5-0 WAMESHINDWA, HATA KUIFUNGA SIMBA ‘HII’ PIA TATIZO?

    DESEMBA mwaka huu Simba na Yanga zitakutana katika mechi ya Nani Mtani Jembe, inayoandaliwa na wadhamini wa klabu hizo, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia Kilimanjaro Premium Lager.
    Tuombe uhai tufike salama, tuone mambo yatakuwaje miamba hiyo ya soka ya Tanzania itakapokutana kwa mara ya pili katika mchezo huo tangu kuanzishwa mwaka jana.
    Utakuwa mchezo wa tatu kwa mwaka huu kuwakutanisha wakongwe hao wa soka ya nchi hii, baada ya ule wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Aprili 19, uliomalizika kwa sare ya 1-1, Haroun Chanongo akitangulia kuifungia Simba dakika ya 76 kabla ya Simon Msuva kusawazisha dakika 10 baadaye na ule wa Jumamosi iliyopita timu hizo zikitoka sare ya 0-0 mzunguko wa kwanza Ligi Kuu msimu huu.

    Na kwa ujumla utakuwa mchezo wa saba tangu Yussuf Manji awe Mwenyekiti wa Yanga SC, timu hiyo inakutana na mahasimu wao hao wa jadi.
    Manji aliingia Yanga SC pamoja na Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga, timu ikitoka kufungwa 5-0 na Simba SC Mei 6, mwaka 2012 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu.
    Kuna imani kwamba kipigo kilikuwa cha hujuma dhidi ya wapinzani wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Yanga SC, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga wakati huo ili kushinikiza aondoke madarakani, na kweli aling’atuka.
    Mchezo wa kwanza Manji akiwa Mwenyekiti Yanga Oktoba 3, 2013 ilitoka sare ya 1-1, Amri Kiemba akitangulia kuifungia Simba SC dakika ya tatu, kabla ya Said Bahanuzi kusawazisha kwa penalti dakika ya 65.
    Mei 18, mwaka 2013,  Yanga ilishinda mabao 2-0, yaliyotiwa kimiani na Didier Kavumbangu dakika ya tano na Hamisi Kiiza dakika ya 62 na huo ndiyo ushindi pekee wa Manji hadi sasa.
    Oktoba 20, mwaka 2013 timu hizo zilitoka sare ya 3-3, Yanga wakitangulia kufunga kipindi cha kwanza mabao ya Mrisho Ngassa dakika ya 15 na Hamisi Kiiza dakika ya 36 na 45, kabla ya Simba SC kusawazisha kipindi cha pili kupitia kwa Betram Mombeki dakika ya 54, Joseph Owino dakika ya 58 na Gilbert Kaze dakika ya 85.
    Desemba 21, Yanga SC ilifungwa 3-1 katika mechi ya Nani Mtani Jembe, mabao ya Simba SC yakifungwa na Amisi Tambwe dakika ya 14 na 44 kwa penalti na Awadh Juma wakati bao la kufutia machozi la timu ya Manji lilifungwa na Emmanuel Okwi dakika ya 87.
    Mechi ya Jumamosi, Yanga SC walikuwa wana matumaini makubwa, si ya kishinda tu, bali kupata ushindi mnono- kwa sababu watani wao walikuwa katika wakati mgumu.
    Simba SC iliingiza timu uwanjani ikiwa na kipa mmoja tu, Peter Manyika tena ambaye ni kipa wa tatu baada ya makipa wa kwanza Ivo Mapunda na wa pili, Hussein Sharrif ‘Casillas’ kuwa majeruhi.
    Lakini pia, wachezaji wengine tegemeo wa Simba SC walikuwa majeruhi, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Miraj Adam, Nassor Masoud ‘Chollo’, Paul Kiongera na Amisi Tambwe.
    Jonas Mkude naye akaumia mchezoni Jumamosi na kutolewa dakika ya 60, lakini bado Yanga haikuweza kufurukuta mbele ya Simba SC iliyokuwa katika ‘hali mbaya’.
    Ni matarajio, kufika Desemba akina Ivo, Casillas, Miraj, Chollo, Baba Ubaya, Mkude, Kiongera na Tambwe wote watakuwa fiti na kocha Patrick Phiri atapanga kikosi kwa utashi wake- maana yake Simba SC itakuwa kamili.  
    Hapo Yanga watarajie nini, ikiwa timu yao imeshindwa kutamba mbele ya Simba SC iliyoonekana kuwa katika wakati mgumu Oktoba 18, mwaka huu.
    Ama kweli Manji kazi anayo Yanga SC, kulipa 5-0 ameshindwa, basi hata kuifunga Simba ‘hii’ tatizo? 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA YA MANJI, KULIPA 5-0 WAMESHINDWA, HATA KUIFUNGA SIMBA ‘HII’ PIA TATIZO? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top