• HABARI MPYA

  Alhamisi, Oktoba 30, 2014

  AZAM FC YAWAFUATA NDANDA FC BILA YA KIPRE TCHETCHE

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KIKOSI cha Azam FC kimeondoka Dar es Salaam mchana wa leo kwenda Mtwara kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji Ndanda FC Jumamosi Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini humo. 
  Lakini katika kikosi hicho beki chipukizi Gardiel Michael na washambuliaji wawili wa kigeni, Kipre Herman Tchetche wa Ivory Coast na Ismaila Diara wa Mali hawamo.
  Meneja wa Azam FC, Jemadari Said Kazumari ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, Michael na Diara ni majeruhi, wakati Kipre Tchetche hajarejea kutoka nchini kwao, Ivory Coast alipokwenda kwa matatizo ya kifamilia.
  Basi jipya la Azam lipo safarini kuelekea Mtwara
  Nahodha Msaidizi wa Azam FC, Salum Abubakar 'Sure Boy' ataiongoza timu mjini Mtwara baada ya kuteuliwa Mchezaji Bora wa Oktoba Ligi Kuu

  Kipre alikwenda kwao, Ivory Coast baada ya mechi dhidi ya Mbeya City mjini Mbeya wiki iliyopita na hakuwepo wakati timu hiyo inafungwa 1-0 na JKT Ruvu Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
  Jemadari amesema wanakwenda Mtwara na kikosi kikubwa, kwa sababu baada ya mchezo huo dhidi ya Ndanda, wanatarajiwa kwenda kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Kariakoo United mjini Lindi. 
  Mabingwa hao watetezi wanaofundishwa na kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog wana pointi 10 baada ya mechi tano, kati ya hizo sare moja, wamefungwa moja na kushinda tatu.
  Azam FC inashika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu, nyuma ya Mtibwa Sugar iliyopo kileleni kwa pointi zake 13 za mechi tano pia, baada ya kushinda michezo minne na sare moja.
  Yanga SC iliyomaliza nyuma ya mabingwa Azam FC msimu uliopita, pia wana pointi 10 baada ya sare moja, kufungwa moja na kushinda mechi tatu, lakini wanakuwa nafasi ya tatu kwa kuzidiwa wastani wa mabao.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM FC YAWAFUATA NDANDA FC BILA YA KIPRE TCHETCHE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top