• HABARI MPYA

  Jumanne, Oktoba 28, 2014

  RANGERS YABISHA HODI KWA FUJO LIGI KUU, YAITANDIKA ASHANTI UNITED 2-1 KARUME

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  TIMU ya Friends Rangers ‘Wakombozi wa Manzese’ leo wamevuna pointi tatu zaidi katika Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara, baada ya kuichapa Ashanti United mabao 2-1 Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
  Shujaa wa Rangers inayofundishwa kiungo wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Ally Yussuf ‘Tigana’ aliyewika Simba SC na Yanga enzi zake, alikuwa ni mshambuliji Mussa John ‘Rooney’ aliyefunga mabao yote hayo.
  Rooney huyo wa Manzese aliifanya Rangers iende kupumzika ikiwa tayari inaongoza kwa mabao hayo mawili, aliyofunga dakika za 25 na 41.
  Wachezaji wa Friends Rangers wakishangilia ushindi wao lei Uwanja wa Karume na chini kushoto ni mfungaji wa mabao hayo Mussa John 'Rooney'.


  Kwa ujumla, Rangers ilicheza vizuri kipindi cha kwanza na kuifunika timu iliyoporomokea Daraja la Kwanza msimu huu kutoka Ligi Kuu, ilikodumu kwa msimu mmoja tu baada ya kupanda msimu uliopita.
  Kipindi cha pili, Rangers inayofundishwa na kiungo wa zamani wa Yanga SC, Maalim Saleh ‘Romario’, Mbaraka Hassan na Mfaume Athumani Samatta aliyewahi kudakia Yanga SC pia, ilibadilika na kuanza kuonyesha upinzani.
  Matunda ya jitihada hizo ilikuwa ni kupata bao la kufutia machozi dakika ya tatu tu tangu kuanza kipindi cha pili, mfungaji Ally Abdallah aliyetumia makosa ya mabeki wa Rangers.
  Mshambuliaji wa Friends Rangers, Yussuf Mgwao akimuacha chini beki wa Ashanti United
  Samuel Mathayo wa Friends Rangers kushoto akiwania mpira dhidi ya mchezaji wa Ashanti
  Mashabiki wa Friends Rangers wakifurahia Uwanja wa Karume leo
  Bao hilo liliizindua Rangers na kuongeza kasi ya mashambulizi kusaka mabao zaidi, hata hivyo hawakufanikiwa kutimiza malengo hayo kutokana na uimara wa Ashanti kipindi cha pili.
  Ushindi huo, unaifanya Rangers itimize pointi 11 baada ya mechi tano sawa na Majimaji ya Songea, ambayo inabaki kileleni kwa sababu ya wastani wa mabao, ikiwa na bao moja zaidi katika Kundi A.
  Ashanti inabaki na pointi sita baada ya mechi tano pia, ikiwa katika nafasi ya nane (kuangalia msimamo nenda http://tff.or.tz).    
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: RANGERS YABISHA HODI KWA FUJO LIGI KUU, YAITANDIKA ASHANTI UNITED 2-1 KARUME Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top