• HABARI MPYA

    Sunday, October 26, 2014

    WAZO LA KUUWEKA UWANJA WA TAIFA KARIBU NA WA UHURU HALIKUWA SAHIHI

    UKARABATI wa Uwanja wa Uhuru, ni kama tayari umekamilika na sasa kinachosubiriwa ni ufunguzi wake tu, ili uanze kutumika baada ya kufungwa kwa zaidi ya miaka mitatu kwa ajili ya ukarabati.
    Huo utakuwa Uwanja wa pili kwa ubora, ukubwa na uzuri nchini, baada ya Uwanja wa Taifa, ambao pia upo Dar es Salaam.
    Na bahati mbaya, au nzuri ni kwamba viwanja hivyo vimepakana kabisa. Uwanja wa Uhuru, ndiyo awali ulikuwa wa Taifa, lakini baada ya ujenzi wa Uwanja mpya mbele ya sekondari ya Jitegemee na kupewa jina Uwanja wa Taifa, wenyewe ndiyo ukapewa jina hilo jipya.
    Ni jambo la kujivunia kwa nchi yetu kupiga hatua hiyo kubwa ya kimaendeleo katika sekta ya michezo- kuwa na viwanja viwili vyenye ubora wa hali ya juu. Ni muongo uliopita tu wakati ambao ilibidi mechi za kimataifa zipelekwe Uwanja wa CCM Kirumba kufuata ubora na ukubwa, lakini leo hali imebadilika.

    Uwanja wa CCM Kirumba ‘haufui dafu’ tena mbele ya Uwanja wa Uhuru na hauingii kabisa mbele ya Uwanja wa Taifa, iwe kwa ukubwa, uzuri na hata ubora.
    Lakini bado CCM Kirumba nao ni Uwanja bora wenye kukidhi vigezo vya kimataifa, wakati huo huo Uwanja Kambarage Shinyanga nao upo kwenye hali nzuri.
    Bado viwanja vingine vya CCM, vinahitaji marekebisho madogo tu vifikie hadhi nzuri, ili idadi ya viwanja vya kimataifa iongezeke nchini.
    Nasema bado viwanja vingine vya CCM vinahitaji marekebisho ili kufikia hadhi ya kimataifa- maana yake hatujawa na viwanja tosha vya kimataifa.
    Kwa Dar es Salaam, pamoja na ukubwa wa mji huu na umaarufu wake, ukamilifu wa ukarabati wa Uwanja wa Uhuru unafanya idadi ya viwanja vitatu vya kibiashara pamoja na Azam Complex, uliopo Chamazi, nje kidogo ya Dar es Salaam, ambao unamilikiwa na klabu ya Azam FC.
    Utaona kitendo cha viwanja vya Taifa na Uhuru na kuwa karibu kinazuia matumizi ya viwanja hivyo kwa pamoja kwa shughuli za soka kibiashara.
    Ukifungua tu mageti ya Uwanja watu waingie, tayari ni gharama ambayo malipo yake ni viingilio ili vikidhi gharama hizo.
    Sasa kama mageti yatafunguliwa na watu wataingia bila malipo kwa sababu wamekwenda kutazama mechi ambayo haina mvuto kibiashara, tutarajie gharama za kuutunza Uwanja huo zitatoka wapi?
    Nchini Kenya,  Jiji la Nairobi lina viwanja viwili vikubwa, bora na vizuri ambavyo ni Nyayo na Moi Kasarani, achilia mbali Uwanja wa Machakos uliopo nje kidogo ya mji.
    Lakini viwanja hivyo havijawekwa karibu karibu kama ilivyo Uhuru na Taifa. Vimetenganishwa, kiasi kwamba vyote vinaweza kutumika kwa wakati mmoja kibiashara.
    Uganda kadhalika, wana viwanja viwili vikubwa na bora, Nakivubo na Mandela, uliopo Namboole ukiachilia mbali viwanja vingine vidogo vidogo lukuki katikati ya mji- lakini havijawekwa karibu karibu.
    Rwanda nao, mjini Kigali pekee wana viwanja viwili vikubwa, Amahoro na Nyamirambo, lakini havijawekwa pamoja kama ilivyo kwa Taifa na Uhuru yetu.
    Tuna kila sababu Watanzania kufurahia kuwa na viwanja bora kama hivyo, Taifa na Uhuru, lakini tukubali wazo la kuviweka pamoja halikuwa sahihi. Alamsiki.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WAZO LA KUUWEKA UWANJA WA TAIFA KARIBU NA WA UHURU HALIKUWA SAHIHI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top