• HABARI MPYA

  Alhamisi, Oktoba 23, 2014

  JKT RUVU WAWEKA KAMBI MOROGORO NA WATAMBA; “JUMAMOSI LAZIMA AZAM AFE”

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  JKT Ruvu imeweka kambi Morogoro kujiandaa na mchezo dhidi ya mabingwa wa Ligi Kuu Azam FC Jumamosi Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam na Sajini Contsantine Masanja amesema; “ushindi lazima”.
  Msemaji huyo wa timu hiyo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) amesema kwamba tangu wametoka Mbeya walipocheza na Prisons Jumamosi iliyopita, wameweka kambi Morogoro kwa ajili ya Azam FC.
  Sajini Masanja ameiambia BIN ZUBEIRY kwamba maandalizi yanaendelea vizuri  na lengo ni kuvunja rekodi ya Azam FC kutofungwa katika mechi 38 za Ligi Kuu.
  “Tuko vizuri na timu inaendelea vizuri na maandalizi, lengo letu ni kushinda dhidi ya Azam ili kujiweka vizuri katika msimamo wa Ligi,”amesema.
  JKT Ruvu imepania kuvunja rekodi ya Azam FC kutofungwa katika mechi 38

  Masanja amesema kwamba JKT itaondoka Morogoro Alfajiri ya Jumamosi kurejea Dar es Salaam tayari kwa mchezo huo jioni yake.
  Amewataja wachezaji ambao wako kwenye hatihati ya kucheza mechi hiyo kuwa ni Furaha Tembo, Issa Kanduru, Lusajo Lautent na Haroun Adolph ambao wote ni majeruhi.
  JKT inayofundishwa na Freddy Felix Isaya Kataraiya ‘Minziro’ au Majeshi, ilipata ushindi wa kwanza katika Ligi Kuu msimu huu Jumamosi baada ya kuichapa Prisons mabao 2-1 Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, baada ya awali kufungwa mara mbili, 2-0 na Kagera Sugar na 2-1 na Yanga na kutoa sare moja na Mbeya City 0-0.
  Na baada ya ushindi huo wa kwanza, JKT inaonekana kupania kuendeleza wimbi la ushindi katika mchezo wake wa keshokutwa na mabingwa hao wa Bara, walio chini ya kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: JKT RUVU WAWEKA KAMBI MOROGORO NA WATAMBA; “JUMAMOSI LAZIMA AZAM AFE” Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top