• HABARI MPYA

    Friday, October 24, 2014

    MBEYA CITY WATAMBA KUIKALISHA MTIBWA SOKOINE

    Na Renatus Mahima, MBEYA
    KOCHA wa Mbeya City, Juma Mwambusi amesema kikosi chake kitasahihisha makosa yaliyokiponza katika mechi iliyopita na sasa kiko tayari kusaka ushindi dhidi ya Mtibwa Sugar mjini hapa keshokutwa.
    Kikianza na washambuliaji wanaosifika kwa kufumania nyavu, Saad Kipanga, Mwagane Yeya na Paul Nonga, kikosi cha Mbeya City kilikubali kupokea kichapo cha 1-0 dhidi ya mabingwa watetezi Azam FC kikiwa ni kipigo cha kwanza msimu huu na cha pili kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine tangu kipande Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita.
    Mwambusi ameiambia BIN ZUBEIRY mjini hapa leo kwamba kikosi chake kilichoanza kwa kusuasua msimu huu kikitoka suluhu dhidi ya JKT Ruvu na Ruvu Shooting, kushinda kwa penalti 1-0 dhidi ya Coastal Union kabla ya kuchapwa na wanalambalamba, kimefanya maandalizi shadidi kwa ajili ya mechi ya kesho dhidi Mtibwa.
    "Tulirejea kambini mara tu baada ya mechi yetu dhidi ya Azam tumesahihisha makosa yaliyojitokeza katika michezo yetu iliyopita tunaamini tutapat matokeo mazuri dhidi ya timu ngumu ya Mtibwa," alisema Mwambusi aliyeibuka kocha bora msimu uliopita.
    Kikosi cha Prisons kitamenyana na Mtibwa Sugar Jumapili 

    Kwa upande wake, Mecky Mexime, kocha mkuu wa Mtibwa Sugar, amesema kikosi chake kilichoingia mjini Mbeya jioni ya leo, kiko vizuri na kitalipa kisasi cha kufungwa 2-1 na wagonga nyundo hao wa Mbeya kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine msimu uliopita.
    "Mbeya City ni timu ngumu kufungika hasa inapocheza nyumbani, lakini hilo halitupi hofu maana tumejiandaa kukabiliana na timu yoyote tunayokutana nayo. Tutakuja Mbeya kusaka matokeo mazuri ili kujiweka pazuri katika msimamo w ligi," alisema nahodha huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar na Taifa Stars.
    Mabingwa wa 1999 na 2000 wa Tanzania Bara, Mtibwa Sugar wko nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo wakizidiwa wa faida ya herufi 'A' katika mtitiriko wa herufi na vinara Azam FC, timu zote zikiwa na pointi 10 baada ya kucheza mechi nne.
    Mbeya City wako nafasi ya sita baada ya kukusnya pointi tano sawa na Kagera Sugar walio nafasi ya tano wakati mabingwa wa Tanzania Bara 1988, Coastal Union wanakamata nafasi ya tatu wakiwa na pointi saba sawa na Yanga wanaoshikilia nafasi ya nne.        
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MBEYA CITY WATAMBA KUIKALISHA MTIBWA SOKOINE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top