• HABARI MPYA

  Jumanne, Oktoba 28, 2014

  HATARI, MCHEZAJI TEMEKE AMCHANJA KIWEMBE MWENZAKE MZANZIBARI COPA COCA COLA, ASHONWA NYUZI 10

  Na Ameir Khalid, ZANZIBAR
  KATIKA hali isiyotarajiwa, mchezaji wa timu ya Mkoa wa Mjini Magharibi (U-15) Ibrahim Abdallah, alijeruhiwa kwa kuchanwa mgongoni mwa wembe na mchezaji wa Mkoa wa Temeke wakati timu hizo zilipopambana Uwanja wa Amaan Jumamosi iliyopita.
  Timu hizo zilikuwa zikiwania tiketi ya kushiriki fainali za michuano ya Copa Coca Cola itakayofanyika baadae jijini Dar es Salaam, ambapo Mjini Magharibi ilishinda kwa mabao 3-0 na kufuzu kutinga hatua ya 16 bora.
  Taarifa zinasema Ibrahim alikutwa na kadhia hiyo wakati zikiwa zimebaki dakika kumi mchezo huo kumalizika na kushonwa nyuzi 10.
  Ibrahim Abdallah akionyesha sehemu aliyoshonwa nyuzi 10 baada ya kuchanjwa wembe a mchezaji wa Temeke 

  Mchezaji wa Temeke Said Mohammed, ndiye anayedaiwa kumchana mwenzake huyo, kwa mujibu wa maelezo yake wakati akihojiwa na viongozi wa timu ya Mkoa wa Mjini Magharibi.
  Katibu wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) Wilaya ya Mjini Yahya Juma Ali, ameelezea kusikitishwa na kitendo hicho, ambacho amesema si cha kimichezo na kingeweza kuleta mzozo mkubwa uwanjani na uvunjifu wa amani.
  Alisema, baada ya kumhoji mchezaji huyo, aliwaeleza kuwa kiwembe hicho alipewa na mmoja wa viongozi wao, ili kutimiza azma hiyo kitendo alichosema hakikupaswa kufanywa na kiongozi wa timu kama hiyo. 
  Katibu huyo alisema kuwa chama chake kinajiandaa kuwasilisha malalamiko yao Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) juu ya kadhia hiyo kuitaka itoe adhabu kali kwa mchezaji huyo na kiongozi aliyempa silaha hiyo.
  "Tutapeleka ripoti na kuiambatanisha na picha za tukio hilo zinazoonesha jinsi kijana wetu alivyojeruhiwa, na tutaiomba TFF kutoa adhabu kali sana kwani kitendo hicho ni sawa na kosa la jinai," alieleza Yahya.
  Hata hivyo, Yahya alisema watu wengi waliwashauri kufungua kesi mahakamani, lakini kwa kuwa hilo ni suala la kimichezo, tumeamua kulipeleka kwa wahusika wa mpira wa miguu ilikotoka timu ya Temeke,  TFF.
  Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu kutoka Dar es Salaam, Msemaji wa TFF Boniface Wambura, alisema bado hawajapokea taarifa hizo, na hivyo asingeweza kulizungumzia suala hilo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: HATARI, MCHEZAJI TEMEKE AMCHANJA KIWEMBE MWENZAKE MZANZIBARI COPA COCA COLA, ASHONWA NYUZI 10 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top