• HABARI MPYA

  Jumatatu, Oktoba 27, 2014

  JERRY TEGETE AMEFUFUA MAKALI, AU ALIWABAHATISHA TU STAND UNITED?

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  BAADA ya mechi ya kirafiki na KMKM Uwanja wa Amaan, Zanzibar Agosti mwaka huu, wachezaji wenzake walimfanyia mzaha Jerry Tegete wa kumpunga mithili ya waganga wa kienyeji.
  Haruna Niyonzima, Hamisi Kiiza na Mrisho Ngassa walihusika katika zoezi hilo kwenye eneo la wachezaji wa akiba.
  Hiyo ilifuatia mshambuliaji huyo kukosa mabao ya wazi mno, Yanga SC ikishinda 2-0 kwa mabao ya Andrey Coutinho na Hussein Javu, moja kila kipindi.
  Ilifikia hata Jerry mwenyewe akajikatia tamaa, na watu wakaanza kumtabiria huu unaweza ukawa msimu wake wa mwisho akiwa na jezi za rangi ya kijani na njano.
  Jerry Tegete katika msimu wake wa pili Yanga SC 2009/2010

  Ikaripotiwa, Tegete alikosa bao la wazi Yanga SC ikicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya CDA mjini Dodoma katikati ya wiki.
  Lakini katika mchezo wa Jumamosi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Tegete alitokea benchi na kufunga mabao mawili Yanga SC ikishinda 3-0 ugenini.
  Mashabiki wa Yanga SC mjini Shinyanga wamevutiwa mno na mabao ya Tegete kiasi cha kusema mtoto huyo wa kocha maarufu mjini Mwanza, John Tegete amefufua makali yake.
  Tegete ni mchezaji ambaye aliibuliwa na kocha wa sasa wa Yanga SC, Mario Maximo alipokuwa anafundisha timu ya taifa, Taifa Stars mwaka 2007 akiwa mwanafunzi wa sekondari ya Makongo, Dar es Salaam.
  Maximo aliamua kumuandaa mchezaji huyo kuwa mkali wa mabao wa nchi baadaye, akimbeba kwenye kambi ya Taifa Stars angali kinda japo, hachezi, mwenyewe akisema anamuandaa.
  Na kweli, baadaye, Tegete akawa mkali wa mabao kuanzia klabu yake, Yanga SC hadi Taifa Stars na mabao yake ndiyo yaliyoipa timu ya taifa tiketi ya CHAN mwaka 2009 nchini Ivory Coast.
  Lakini kwa misimu mitatu iliyopita, Tegete akapoteza makali yake kiasi cha umaarufu wake kufifia pia.
  Jumamosi ameshangilia mabao mara mbili Shinyanga na Jumamosi ijayo, Yanga SC itacheza mechi ya pili mfululizo ugenini itakapomenyana na Kagera Sugar Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.
  Bao lake la kwanza kabisa Ligi Kuu baada ya kusajiliwa Yanga SC msimu wa 2008/2009 Tegete alifunga dhidi ya Kagera mjini Bukoba.
  Yanga SC ilikuwa tayari imekwishajihakikishia ubingwa na ikapanda ndege kwenda Bukoba kucheza mechi ya kuhitimisha kalenda na kuchapwa mabao 3-1, bao la kufutia machozi akifunga mtoto wa kocha Tegete.
  Na Tegete alifanikiwa kurudia kufunga Uwanja wa Kaitaba, kabla ya makali yake kupotea miaka ya karibuni. Je, Tegete amefufua makali, au aliwabahatisha tu Stand United?  Mechi zijazo zitatoa majibu. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: JERRY TEGETE AMEFUFUA MAKALI, AU ALIWABAHATISHA TU STAND UNITED? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top