• HABARI MPYA

  Jumatatu, Oktoba 27, 2014

  LUNDENGA KUNA WANA WANAHARAMU WENGINE HAWAPITI HATA UFUNIKE KOMBE KWA KIASI GANI

  HASHIM Lundenga mkurugenzi wa Lino International Agency inayoaandaa mashindano ya urembo ya Miss Tanzania, ni mtu ninayemkubali sana katika suala la kujenga hoja na kupangua changamoto za waandishi wa habari, ni aina ya mtu ambaye utapenda kumsikiliza tena na tena.
  Lakini nikiri kuwa kwa mara ya kwanza ameniangusha - Lundenga ameniangusha kwa namna alivyohodhi mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika wiki iliyopita ambapo pamoja na mambo mengine, suala la utata wa umri wa Miss Tanzania 2014, Sitti Abbas Mtevu lilichukua nafasi.

  Kabla sijasonga mbele, napenda niwajulishe kuwa kwa vyanzo vyangu binafsi ikiwemo ndani ya Idara ya Uhamiaji Tanzania, nimejiridhisha kuwa hati ya kusafiria iliyozagaa mitandaoni inayoonyesha kuwa Sitti amezaliwa mwaka 1989, si sahihi na hiyo inanifanya niamini kuwa cheti cha kuzaliwa cha Sitti kilichotengenezwa mwezi Septemba mwaka huu kikionyesha kuwa amezaliwa mwaka 1991, ni feki.
  Kwa hali hiyo, Sitti anapoteza sifa za kibalozi ambayo ni moja ya vigezo vikubwa vinavyohitajika kwenye kinyang’anyiro cha Miss Tanzania – Utakuweje na sifa za kibalozi huku ukiwa kinara wa kughushi nyaraka muhimu kama hizo? Tumewahi kushuhudia watu waking’olewa kwenye michakato ya uchaguzi wa vyama vya siasa na hata vyama vya michezo kwa sababu ya kughushi vyeti vya shule – Sitti hatofautiani kabisa na watu hao.
  Katika mkutano huo wa waandishi wa habari, Sitti alionyesha cheti chake cha kuzaliwa lakini alipohojiwa kuhusu hati yake ya kusafiria, Sitti akasema hawezi kujibu mambo ya mitandao na kwamba yeye amekwenda kuzungumzia kuhusu cheti chake cha kuzaliwa tu.
  Siiti alionyesha kupoteza sifa nyingine ya kibalozi kwa kujibu maswali kwa jazba tena kwa upeo wa kiwango cha chini mno – Unapoolizwa cheti chako kilipopotea uliripoti wapi halafu ukasema hukujiandaa kujibu swali hilo, linakuwa ni jambo la kitoto kuliko hata utoto wenyewe.
  Unapowaambia waandishi wa habari eti mmekuwa mkiniandama sana kwa mambo mengi ambayo mengine si ya kweli maanake ni nini? Maanake ni kuwa kati ya hayo yapo ya ukweli, hakika Sitti ameonyesha uwezo mdogo sana wa kukaa mbele ya waandishi na kujibu hoja, ni mweupe sana.
  Kwanini nimesema Lundenga ameniangusha? Ni kwa sababu alimlinda Sitti asijibu maswali ya msingi, hakutaka kumbana Sitti atumie fursa hiyo kusafisha ukungu wote uliomzunguka, inakuweje Sitti akatae kujibu swali kuhusu cheti chake cha zamani kilichomwezesha kupata hati ya kusafiria? Tena Sitti anasema kwa macho makavu: “SIWEZI KUJIBU HILO SWALI” kisha Lundenga anamkingia kifua.
  Kama cheti cha zamani ndicho kilichompatia hati ya kusafiria Sitti, hati inayoonyesha kuwa ana umri wa miaka 25 ambao ni nje ya umri unahitajika Miss Tanzania na hata Miss World, basi Lungenga pia angehitaji kusikiliza majibu ya msingi kuhusu hoja hiyo na si kulikwepa swali.
  Kulikwepa swali hili muhimu ni sawa na kufunika kombe mwanaharamu apite, lakini napenda kumjulisha Lundega, Sitti na washika dau wengine kuwa wako wanaharamu wengine huwa hawapiti nata ufunike vipi kombe.
  Ukibahatika kupitia maandishi ya watu kama Godsos Mukama (Mwandaaji wa Miss Mara) na William J Malecela (mmoja wa waandaji wa Miss Ilala), utagundua kuwa hata watu walioko jikoni nao pia hawaiungi mkono kamati ya Miss Tanzania juu ya uhalali wa Sitti kutwaa taji. 
  Ushindi wa Sitti umezongwa na mambo mengi yenye utata - Ndugu, jamaa na mashabiki wake kuingia na mabango yenye maandishi makubwa SITTI, ilikuwa ni jambo ambalo sikumbuki kuwahi kuliona kabla ya shindano la mwaka huu, haya ni mashindano ambayo hata kwenda kumtunza pesa mshiriki jukwaani huwa haikubaliki kwa vile inaweza ikawavuruga majaji, inakuweje mabango kama yale yatawale ukumbini?
  Tunaambiwa Sitti ajibu kwa lugha mbili – kiingereza na kifaransa, tunajua wazi kuwa lugha zinazotumika katika ngazi zote za Miss Tanzania ni Kiswahili na Kiingereza, hiki Kifaransa kilitokea wapi? Yaani mshiriki anaulizwa atajibu kwa lugha gani, akachagua Kiingereza lakini baada ya kumaliza kujibu akasema “Najibu na kwa Kifaransa” … mtoto wa kike akatiririka.
  Kwa kuangalia ‘fujo’ zote hizo za Sitti pamoja na tuhuma za rushwa zilizotajwa juu ya ushindi wake, Lundenga alistahili kumwacha Sitti ajibu kila utata uliostahili majibu, kumlinda Sitti na maswali ya wanahabari kunaweza kuwafanya watu wahisi vitu vya ajabu.
  Mwisho napenda kuitahadharisha kamati ya Miss Tanzania kuwa hilo liwe funzo kwao, ipo haja ya kupitia nyaraka nyingi za washiriki kuanzia vyeti vya kuzaliwa, vitambulisho vya kupigia kura, passport na leseni za kuendeshea gari (kwa wenye nazo) ikibidi hata vyeti vya shule. Tukumbuke kwenye soka letu, Tanzania tuliwahi kuporwa nafasi ya kushiriki fainali za Afrika kwa vijana kwasababu ya umri wa mchezaji mmoja tu, suala la umri ni nyeti sana, tusiishie kufunika kombe mwanaharamu apite.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: LUNDENGA KUNA WANA WANAHARAMU WENGINE HAWAPITI HATA UFUNIKE KOMBE KWA KIASI GANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top