• HABARI MPYA

    Monday, October 06, 2014

    DAKTARI SIMBA SC AELEZEA MAUMIVU YA OKWI…NA ASEMA IVO MAPUNDA ANAANZA KUJIFUA KESHO

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    DAKTARI wa Simba SC, Yassin Gembe amesema kwamba mshambuliaji, Mganda Emmanuel Okwi aligongwa kwenye enka na goti katika mchezo wa juzi dhidi ya Stand United, lakini yuko fiti kabisa kucheza Oktoba 18, dhidi ya Yanga SC.
    Simba SC Jumamosi ilitoa sare ya 1-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Stand iliyopanda Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu.
    Katika mchezo huo, Okwi alitolewa nje mara mbili kupatiwa huduma ya kwanza na Dk Gembe, lakini mara zote alirejea uwanjani kuendelea na mchezo.
    Pigo la pili lilimfanya mchezaji huyo wa zamani wa Yanga SC aendelee kucheza huku akichechemea, hali ambayo ilizua hofu labda amepata maumivu makubwa.
    Daktari wa Simba SC, Yassin Gembe akimtibu Okwi juzi


    “Ni kweli Okwi aligongwa mara mbili, mara moja kwenye enka na mara moja kwenye goti. Lakini hayakuwa maumivu makubwa na kesho ataendelea na mazoezi,” amesema Gembe.
    Wachezaji wa Simba SC watakuwa na siku nyingine ya mapumziko leo, kabla ya kesho kuanza tena mazoezi kujiandaa na mchezo dhidi ya mahasimu, Yanga SC Oktoba 18.
    Aidha, Dk Gembe amesema kwamba kipa Ivo Mapunda na beki Nassor Masoud ‘Chollo’ wataanza mazoezi ya kujiweka fiti wiki hii.
    Ivo aliumia kidole na anatakiwa kuwa nje kwa wiki nane, hivi sasa akiwa yupo katika wiki ya tatu, wakati Chollo aliyeumia mkono, anatakiwa kuwa nje kwa wiki tatu, hivi sasa akiwa anaingia katika wiki ya pili.
    “Hawa wachezaji maumivu yao hayawazuii kufanya mazoezi ya kujiweka fiti, kwa hivyo niliwapa mapumziko mafupi kabla ya kuanza mazoezi ya kukimbia na gym. Ivo nilimpa wiki mbili za kupumzika na Chollo wiki moja, kwa hivyo wote wiki hii wataanza mazoezi,”amesema Gembe.
    Gembe pia amesema wachezaji Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ na Haroun Chanongo ambao wiki iliyopita walifanya mazoezi mepesi, nao kesho wataanza mazoezi kikamilifu na wenzao.
    Majeruhi mwingine wa muda mrefu Simba SC ni Mkenya, Paul Kiongera ambaye anatakiwa kuwa nje kwa wiki sita baada ya kuumia goti, hivi sasa akiwa katika wiki ya nne- na Dk Gembe amesema ‘fowadi’ huyo anaendelea vizuri. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: DAKTARI SIMBA SC AELEZEA MAUMIVU YA OKWI…NA ASEMA IVO MAPUNDA ANAANZA KUJIFUA KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top