• HABARI MPYA

    Sunday, July 07, 2013

    ANGALIA AZAM, WAGEUKIE YANGA SC NA TABIRI NINI KITATOKEA MWAKANI

    IMEWEKWA JULAI 7, 2013 SAA 11:23 ALFAJIRI
    MWAKA huu Azam FC ilishiriki kwa mara ya kwanza michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na ikakaribia moja kwa moja kutinga hatua ya makundi, kama si kutolewa kwa mbinde na AS FAR Rabat ya Morocco katika hatua ya tatu ya michuano hiyo.
    Azam FC ilitolewa kwa jumla ya mabao 2-1 na Waarabu hao, kufuatia kutoka sare ya 0-0 Dar es Salaam kabla ya kwenda kufungwa 2-1 ugenini wiki mbili baadaye kati ya Aprili na Mei mwaka huu.

    Baada ya sare ya bila kufungana Uwanja wa Taifa, Azam ilihitaji angalau sare yoyote ya mabao ili kusonga mbele na katika mchezo wa marudiano, zikiwa zimesalia dakika nane, wakiwa nyuma kwa mabao 2-1, walifanikiwa kupata penalti, lakini John Bocco ‘Adebayor’ akaenda kugongesha mwamba wa juu.
    Na siku hiyo, Azam ilicheza pungufu kwa wachezaji wawili, baada ya mabeki Waziri Salum na David Mwantika kutolewa nje kwa kadi nyekundu. Awali, Azam iliitoa Al Nasir Juba ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 8-1, na baadaye Barack Young Controllers II ya Liberia kwa mabao 2-1.
    Ikishiriki kwa mara ya kwanza, Azam ilionyesha imejiandaa kiasi cha kutosha kwa ajili ya kushindana na ilichukua tahadhari ya kutosha. Kila kabla ya mechi ya ugenini, ilikuwa ikitanguliza Maofisa wake kwenda nchi wanayotarajiwa kucheza kwa ajili ya kuandaa mazingira mazuri ya timu kufikia na kufanya mazoezi, ili kuepuka hujuma za wenyeji.
    Mambo kama hayo hufanywa na timu nyingine zote zenye nia ya kushindana zinapokuja hata hapa nyumbani- na mwaka huu tumeona Recreativo de Libolo ya Angola ilipokuja kucheza na Simba katika Ligi ya Mabingwa ikitanguliza watu wake kuandaa mazingira.
    Kwa ufupi ni kwamba, Azam ni timu yenye mipango ambayo inakosekana kwa vigogo wa soka nchini Simba na Yanga.
    Yana SC walikuwa wana timu nzuri sana baada ya msimu wakitwaa mataji mawili, Kombe la Kagame na Ligi Kuu na kilichoonekana timu ilihitaji tu kuongeza mshambuliaji mmoja mwenye uwezo mkubwa na ubunifu zaidi kuliko waliokuwepo.
    Lakini hadi sasa, Yanga imekwishasajili wachezaji wapya zaidi ya sita na ndani yake mshambuliaji ni mmoja tu na tena chipukizi, Shaaban Kondo, ambaye dhahiri hawezi kwenda kuwapiku haraka Jerry Tegete na Didier Kavumbangu.
    Mshambuliaji aliyekuwa ana ahueni kidogo msimu uliopita, Hamisi Kiiza anaweza akakosekana msimu ujao baada ya kumaliza Mkataba wake na majadiliano ya kuongeza Mkataba yanaelekea kuwa magumu. Kiiza anataka dola za Kimarekani 40,000, Yanga wanataka wampe dola 35,000 na 5,000 nyingine wampe gari. Yeye hataki.
    Huwezi kuona mantiki ya Yanga SC kuwaacha wachezaji wake wengine wazoefu kama Said Mohamed, Godfrey Taita, Stefano Mwasyika na Nurdin Bakari. Kweli hawakuwa na namba katika kikosi cha kwanza msimu uliopita, kwa sababu waliokuwa wakipangwa ni chaguo la kocha.
    Nurdin ni mchezaji ambaye anaweza kucheza nafasi yoyote na ana miaka hata mitano mbele ya kuendelea kucheza soka ya ushindani, ingawa kweli kwa sasa anatendewa haki kusugua benchi mbele ya viungo kama Frank Domayo, Athumani Iddi ‘Chuji’ na Haruna Niyonzima.
    Lakini bado ukiwa na mtu kama huyu katika timu yako, unakuwa na mchezaji wa maana na aliye tayari kucheza mechi za mashindano na kwa hulka ya Nurdin soka yake iko juu wakati wote.
    Nenda kwa kipa Said, mabeki Mwasyika na Taita, wote hawa waliingia Yanga SC wakiwa wachezaji wa timu ya taifa na msimu uliotangulia kabla ya uliomalizika walikuwa tegemeo katika kikosi cha kwanza timu ikitwaa Kombe la Kagame na kushika nafasi ya tatu Ligi Kuu kwa ‘kutaka wenyewe’. 
    Kwa kukosa namba Yanga, wakapoteza na namba zao timu ya taifa na sasa wanapotezwa zaidi kwa kuachwa kabisa katika timu. Sasa tafakari wanaachwa hao, wanasajiliwa akina nani na kwa vigezo vipi?
    Mapema tu baada ya msimu, kocha Muingereza wa Azam FC alisema hatasajili mchezaji yoyote hadi mwishoni mwa mwaka kwa sababu wakati huo atakuwa anafanya na usajili wa michuano ya Afrika pia.
    Anataka kuitathmini timu katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu na baada ya hapo akiona anahitaji kuongeza nguvu atafanya hivyo. Hapa Stewart kwa lugha nyingine ni kwamba hataki kuitia timu hasara anataka ikisajili mchezaji, basi awe ni hitaji kweli.
    Achana na hayo, elekea kwenye maandalizi ya timu kwa ajili ya msimu mpya. Yanga SC waliposikia kuna kwenda kutetea Kombe lao la Kagame walijipanga kufanya mazoezi kwa wiki mbili kabla ya kwenda kwenye michuano hiyo.
    Lakini ndani ya wiki moja ya kuwapo kwao mazoezini, wakasikia Sudan hakuna amani na Serikali ikatoa tamko timu za Tanzania zisiende, Yanga wakavunja kambi haraka sana, tena siku ya pili yake tu, na kutangaza kuanza tena Julai 2, mwaka huu, kocha wao Ernie Brandts akapanda ndege kurejea Uholanzi.
    Wamefanya mazoezi kwa siku tatu kuanzia Julai 2, tayari wako Kanda ya Ziwa wanacheza mechi za kirafiki. Shamte Ally alikuwa mchezaji mzuri sana, lakini desturi ya kuipa timu mechi za kujipima nguvu kabla wachezaji hawajawa fiti kwa mazoezi ndiyo leo inamtesa akiwa ametemwa kwenye kikosi cha timu hiyo, kwani aliumia na akashindwa kurudi katika kiwango chake.
    Mwaka jana, Yanga SC walifanya programu nzuri ya maandalizi ya msimu, wakianzia kwa mazoezi ya ufukweni, lakini mwaka huu wamekwenda moja kwa moja sekondari ya Loyola ‘kupiga ndiki’.
    Rahisi tu, Yanga SC hawafanyi kitu hadi Simba wafanye na kwa sababu Wekundu wa Msimbazi hawajakwenda Coco Beach hadi sasa, hata Wana Jangwani wanaona haina maana.
    Huwezi hata kufikiria kwamba eti Yanga SC wana programu mbovu, hapana, bali ni bora liende na haitakuwa ajabu msimu ujao ukiwa mgumu kwao, kwa sababu wapinzani wao Simba SC baada ya msimu mbaya uliopita, wametulia na wanajipanga.
    Wamekuwa mazoezini kwa takriban mwezi mzima sasa na tayari kocha mpya, Alhaj Abdallah Athumani Sief ‘King Kibadeni’ ana programu nzuri ya mwendelezo wa maandalizi kwa michezo ya kirafiki baada ya wachezaji kuwa fiti.
    Na bado timu kama Coastal Union ya Tanga, Mtibwa Sugar ya Morogoro nazo zinaonekana kujipanga vizuri kwa ajili ya kuleta ushindani katika Ligi Kuu msimu ujao.
    Kuelekea michuano ya Afrika mwakani, Tanzania itawakilishwa na Yanga katika Ligi ya Mabingwa na Azam Kombe la Shirikisho, unaweza kutabiri nini hapa?
    Rahisi sana mtu kushawishika na Azam kwamba watafanya vizuri kwa sababu ya mipango na programu zao nzuri, zisizo za bora liende.
    Usisahau, wanafanya mazoezi katika Uwanja mzuri wa Azam Complex kule Chamazi, tofauti na Yanga SC ambao wanafanya mazoezi katika Uwanja ambao kocha wao tu amekwishasema si mzuri na hauwezi ukamsaidia kuwa na timu nzuri. Haya waungwana, niwatakie Jumapili njema, tukijaaliwa Jumatano tena.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: ANGALIA AZAM, WAGEUKIE YANGA SC NA TABIRI NINI KITATOKEA MWAKANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top