• HABARI MPYA

    Sunday, January 17, 2016

    BUSARA INAHITAJIKA SUALA LA UHAMISHO WA SAMATTA, VINGINEVYO…

    KATIKA wakati ambao anapaswa kufurahia mafanikio yake ya khistoria, akiwa na klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), mshambuliaji Mbwana Ally Samatta amejikuta ‘anaumwa kichwa’ kwa msongo mawazo.
    Samatta amemaliza mwaka vizuri, akishinda Kombe la Afrika, ufungaji bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika na kutwaa tuzo ya Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika.
    Lakini baada ya hapo, akiwa anaelekea kumaliza Mkataba wake Mazembe, linatokea suala la uhamisho kueleka Ulaya, huku klabu mbili zikitajwa kuwania saini yake.
    Hizo ni KRC Genk ya Ubelgiji na Nantes ya Ufaransa na hapo ndipo unapotokea msongo wa mawazo wa Samatta kutokana na kutofautiana na mmiliki wa Mazembe, bilionea Moise Katumbi juu ya klabu gani aende.

    Samatta anataka kwenda Genk na inasemekana amekwishasaini nayo Mkataba wa awali – lakini Katumbi anataka mchezaji wake aende Nantes.
    Samatta ni mali ya Mazembe hadi Aprili atakapokuwa huru wakati ambao hakuna dirisha lolote la usajili litakuwa wazi hadi Agosti.
    Kusubiri kwa takriban mwaka mzima ndipo akaanze kucheza Ulaya ikiwa atashikilia msimamo tofauti na Katumbi, au kumsikiliza bosi wa klabu yake ya sasa ili hata wiki ijayo aanze kucheza Ulaya – hiyo ni sawa na kusuka au kunyoa kwa Samatta.
    Maamuzi ya Samatta kwa sasa yanatokana na watu wake wa karibu, hususan Meneja wake, Jamal Kisongo ambaye kwa hakika amemuongoza vizuri kijana kufikia hapa.
    Lakini bahati mbaya, wametokea wapambe zaidi ambao sifa zao ni kuvamia mafanikio ya watu na kujiweka kimbelembele kana kwamba wana mchango wowote kwenye historia ya mafanikio ya mtu.
    Na hao sasa ndiyo wanaochangia msongo wa mawazo wa Samatta, wakiwa hawana ujuzi wowote wa masuala ya uhamisho wala uzoefu wa njia za mafanikio ya wachezaji weusi Ulaya sasa wanaonekana kuwa washauri wakuu na hata wazungumzaji pia.
    Nimesoma habari, sijui makala moja jana kwenye tovuti moja, ikimtuhumu Katumbi eti anafanya hila kwa kushirikiana na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Samatta asiende Ulaya.
    Nianze kwa kusema uandishi wa habari mgumu – una miiko na maadili achilia mbali mwongozo, vitu ambavyo siku hizi havizingatiwi sana na ndiyo maana habari nyingi siku hizi si habari, bali ni maelezo tu.
    Mwandishi anajihatarisha kwa kumbebesha tuhuma nzito Katumbi, ambazo bila shaka mmiliki huyo wa Mazembe akiamua kuchukua hatua za kisheria itakuwa hatari.
    Kusema Katumbi aliamua kwenda kusuka dili na Nantes nchini Ufaransa baada ya kuona Samatta na Genk wamefikia pazuri ili kuzuia mpango wao ni tuhuma nzito, ambazo inahitaji ushahidi kuziandika na si dhana tu.
    Kusema TFF inashirikiana na Katumbi kukwamisha mpango wa Samatta kwenda Genk, ni tuhuma nyingine nzito ambazo moja kwa moja zinaichafua bodi hiyo ya soka nchini.
    Sitaki kuamini kuna mtu ndani ya TFF anaweza kushiriki mpango wowote wa kukwamisha ndoto za Samatta – lakini pia wakati wote vyema tukawa wapembuzi yakinifu wa mambo kuliko kuwa watu wa kukurukupa.
    Miaka minne iliyopita Samatta alikuwa nani? Alikuwa ana ndoto gani na nani alikibaini kipaji chake na kwenda kukipambanua kimataifa kama si Mazembe ya Katumbi?  
    Leo Samatta atasifiwa na kutukuzwa sana kwa sababu tu ya mafanikio yake kiasi kwamba watasahaulika hata wale walio nyuma ya mafanikio yake. 
    Gazeti kubwa la michezo nchini Ufaransa, Lequipe limeandika habari za Samatta kutakiwa na Nantes na limemnukuu Rais wa klabu hiyo – leo unaanzaje kusema Katumbi anacheza dili chafu?
    Pamoja na yote, katika kikao cha pamoja baina ya mwakilishi wa Nantes na Meneja wa Samatta, Kisongo kuna makubaliano yalifanywa kutokana na hofu hiyo inayozushwa eti Katumbi anacheza dili na klabu ya Ufaransa kumhujumu nyota wa Tanzania.
    Kisongo pamoja na kufikia makubaliano ya maslahi binafsi ya Samatta ikiwemo dau la kusaini, mshahara, masharti na marupurupu mengine, alitaka kiwepo kipengele cha mchezaji kutorejeshwa Afrika iwapo hatapata nafasi ya kucheza Nantes, bali auzwe klabu nyingine ya Ulaya. Nantes walikubali.
    Nantes ilionyesha nia ya dhati kabisa ya kumchukua Samatta na Kisongo aliinuka kwenye meza ya mazungumzo akiwa amekubali na kusema anakwenda kuzungumza na mchezaji.
    Hata hivyo, inaonekana Samatta mwenyewe ndiye anayetaka kwenda Ubelgiji na si Ufaransa, kwani kitendo cha Kisongo kutorejesha majibu kwa Nantes kinaashiria ameshindwa kumshawishi mchezaji wake akubali ofa hiyo.
    Na hapa sasa ndipo mchezaji mwenyewe anapojiweka katika wakati mgumu wakati jambo lenyewe si gumu kiasi hicho. Lilipofikia suala la Samatta ni la kibiashara zaidi na wakala anayehangaikia mpango wa KRC Genk kwa sasa anajali zaidi muda na gharama zake alizopoteza katika suala hilo.
    Wakala atapenda kutengeneza mpango hata wa Samatta kusubiri amalize Mkataba Aprili ili akaanze kucheza msimu ujao Ulaya, ili mradi tu apate fungu lake. Si mbaya, kikubwa uzima tu.
    Lakini Kisongo anasahau kwamba mapema mwezi huu amepeleka vijana wawili, beki Abuu Ubwa na kiungo Haroun Chanongo Mazembe kwa majaribio huku akiwa na mpango wa kumpeleka Ibrahim Hajib pia.
    Kwa kifupi, hata TFF inapenda kuona Mazembe linakuwa daraja zuri la wachezaji wa Tanzania kwenda Ulaya, kwa sababu hata Thomas Ulimwengu naye yuko njiani kwenda huko.
    Na TFF inapenda mahusiano mazuri na Mazembe yadumu kwa matarajio ya kuwa daraja la vijana wetu kwenda Ulaya.
    Hilo silo ambalo anatazama yule wakala ambaye ametumia muda mrefu kumtafutia soko Samatta Ulaya, yeye anataka mchezaji aondoke Lubumbashi kwa vyovyote, ili mradi tu apate fungu lake.
    Kama tunaamini Samatta akienda Ulaya tu atakuwa amefungua milango ya wachezaji wengine wa Tanzania kwenda huko, tutakuwa tunajidanganya kwa sababu inahitaji kupitia klabu aina ya Mazembe kucheza mechi nyingi kubwa kama Samatta ili kufikia uwezo wa kucheza Ulaya.
    Unahitaji kucheza Ligi ngumu kama ya DRC na kisha ucheze michuano ya Afrika kuanzia hatua za awali, makundi na angalau Nusu Fainali ili kufikia kuzungumziwa wa kucheza Ulaya. 
    Huwezi kumtoa Hajib moja kwa Simba SC umpeleke Ulaya useme atafuzu, labda ligi ndogo ndogo na za nchi ndogo ndogo pia.     
    Rais wa Nantes ya Ufaransa, Waldemar Kita amekaririwa akielezea masikitiko yake juu ya Samatta kukataa ofa ya kujiunga na klabu yake, lakini hajakata tamaa kwa sababu kijana huyo bado ni mali ya TP Mazembe.
    “Tungependa kumpata. Inavyoonekana amesaini (KRC Genk). Lakini ni mali ya klabu gani? Atakuwa huru mwishoni mwa msimu? Mawakili wangu wanalishughulikia hilo suala kwa siku mbili, au tatu,”. 
    “Kama itakuwa poa, au hapana, vizuri, mbaya sana, yote maisha,” amesema katika safu ya Ocean Press.
    Pamoja na maelezo haya ya Kita, bado unaweza kusema Nantes ni mpango hewa?
    Tuipokee hofu iliyopo na tusiipuuze, basi tuiwekee kinga ya kisheria kwa mfano kusaini vipengele ambavyo vitaibana Nantes. Mbona inawezekana!
    Hapa suala ni Samatta kucheza Ulaya katika klabu ambayo atapata maslahi mazuri na fursa ya kucheza, lakini pia tuzingatie kwamba hata huyo Katumbi hafanyi masihara pale Mazembe, anafanya biashara, tena ya uwekezaji usio na uhakika wa faida.
    Wakati anamchukua Samatta kutoka Simba SC miaka minne iliyopita, nani alijua kama atafanikiwa? Lakini aliamua kwa sababu tayari amekwishaamua kufanya biashara hiyo.
    Ikumbukuwe Samatta aliondoka Simba SC pamoja na kiungo Mganda, Patrick Ochan ambaye alipewa nafasi zaidi ya kung’ara Lubumbashi.
    Lakini mambo yamekuwa tofauti, ni Samatta ndiye aliyefanikiwa. Ulimwengu leo ni mchezaji mkubwa pia kati ya wachezaji wanaocheza barani hapa, lakini aliingia Mazembe kama mchezaji wa timu ya vijana. Tumesahau?
    Ukweli ni kwamba busara ya hali ya juu inahitajika katika suala la uhamisho wa Samatta. Wasalam. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BUSARA INAHITAJIKA SUALA LA UHAMISHO WA SAMATTA, VINGINEVYO… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top