• HABARI MPYA

  Sunday, May 05, 2024

  GUEDE AWEKA BAO PEKEE YANGA YAIKANDA MASHUJAA 1-0 KIGOMA


  MABINGWA watetezi, Young Africans wamezidi kulikaribia taji la tatu mfululizo la Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara na la 30 jumla baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Mashujaa FC leo Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.
  Shukrani kwa mfungaji wa bao hilo pekee mshambuliaji Muivory Coast, Joseph Gnadou Guede dakika ya 41 akimalizia pasi ya kiungo mzawa, Mudathir Yahya Abbas baada ya kazi nzuri ya kiungo mshambuliaji Mburkinabe, Stephane Aziz Ki.
  Kwa ushindi huo, Yanga inafikisha pointi 65 katika mchezo wa 25 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi 11 zaidi ya Azam FC inayofuatia ingawa ina mechi moja mkononi na kesho inacheza na Mtibwa Sugar Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro.
  Kwa upande wao Mashujaa FC baada ya kupoteza mchezo wa leo wanabaki na pointi zao 23 za mechi 25 sasa nafasi ya 14 kwenye Ligi ya timu 16.
  Ikumbukwe timu mbili za mwisho zitashuka Daraja mwisho wa msimu na mbili zitamenyana zenyewe nyumbani na ugenini ili mshindi wa jumla asalie Ligi Kuu wakati timu itakayofungwa itakwenda kucheza na timu kutoka Championship kujaribu tena kubaki Ligi Kuu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: GUEDE AWEKA BAO PEKEE YANGA YAIKANDA MASHUJAA 1-0 KIGOMA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top