• HABARI MPYA

  Saturday, July 15, 2023

  SASA PAMBA FC MALI YA HALMASHAURI YA JIJI LA MWANZA  HALMASHAURI ya Jiji la Mwanza jana ilipokea barua rasmi ya kukabidhiwa na kuiendesha  timu ya Pamba FC maarufu kama TP Lindanda kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza baada ya mchakato wa umiliki kutoka bodi ya Pamba na kuletwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kukamilika.
  Akizungumza jana na wadau wa michezo kwenye ukumbi mkubwa wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa,Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.CPA Amos Makalla amebainisha Mkoa huo una kila sababu ya kuwa na timu ya Ligi kuu kutokana na historia yake nzuri ya kuwa na vipaji vya soka na miundombinu bora ya viwanja.
  Amesema baada ya kukabidhiwa rasmi timu ya Pamba kwa barua alikutana na uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza chini ya Mkurugenzi Aaron Kalugumjuli na kuwauzia wazo la kuimiliki na kuiendesha na walikubali kwa mikono miwili,hivyo leo baada ya kikao hicho atamkabidhi naye rasmi kwa barua.


  "Ndugu zangu nimewaita hapa wengi wenu mnajua mimi ni mdau kindaki ndaki wa soka nikianzia kuucheza kwa muda mrefu katika mpira wa kisasa huwezi kufanikiwa kwa vimichango vidogo vidogo ni lazima sasa tuingie katika sura mpya sitakuwa nautendea haki Mkoa huu kama tutakosa timu ya Ligi Kuu",amesisitiza CPA Makalla.
  Katika Mkutano huo uliohudhuriwa na viongozi wa Chama cha Soka Mwanza na uongozi wa timu ya Pamba,Mkuu huyo wa Mkoa amehimiza mchakato wa kuundwa kamati ya mpito kwa lengo la kukamilisha hatua zote muhimu za usajili na mapendekezo ya kocha wachezaji gani wabaki na nani wakuwachwa yafanyike haraka.
  " Tuutumie muda huu mchache vizuri kuanzia marekebisho ya benchi la ufundi,na tuangaze baadhi ya wachezaji bora wa Ligi kuu waje kuchanganyika na hawa ili tupate timu imara itakayo kuja kuutoa kimaso maso Mkoa wa Mwanza," amehimiza Mkuu huyo wa Mkoa.
  "Sisi kama viongozi wa soka Mkoani hapa,hatua hii imetufariji na mwanga wa kucheza Ligi kuu tunauona, hasa ikizingatiwa kuendesha timu kwa mafanikio kuna hitaji fedha nyingi," Vedasto Lufano,M/kiti MZFA.
  "Hadi leo tulikuwa tumejichangisha Shs Milioni 14 kwa ajili ya kuiendesha timu msimu huu,lakini kwa taarifa hii timu ya kuwa chini ya Halmashauri ni dhahiri tutafika mbali,tunakushukuru mno Mhe. Makalla,"Evaristi Hagilla,M/kiti Klabu ya Pamba
  Kwa zaidi ya miaka 20 timu ya soka ya Pamba haijashiriki Ligi Kuu licha ya kutamba miaka ya 90 na kutoa wachezaji wengi waliong'ara kwenye vilabu vikubwa vya Simba na Yanga akiwemo George Masatu.Hussein Marsha,John Makelele na Fumo Felician.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SASA PAMBA FC MALI YA HALMASHAURI YA JIJI LA MWANZA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top