• HABARI MPYA

  Saturday, July 15, 2023

  JEZI MPYA ZA SIMBA KUZINDULIWA MLIMA KILIMANJARO IJUMAA


  JEZI mpya za klabu ya Simba zitazinduliwa katika kilele cha Mlima Kilimanjaro Ijumaa wiki hii.
  Akizungumza katika tafrija maalum ya kutambulisha uhusiano wao na benki yao ya NMB, Mtendaji Mkuu wa Simba, Imani Kajula amesema kwamba jezi hiyo itaanza kupandishwa mlimani Jumatano na watakuwa kileleni siku ya Ijumaa na Jumamosi jezi itakuwa kwenye maduka yote nchini.
  "Simba itazindua jezi zake juu ya mlima Kilimanjaro, kwani hii inaendana na ukubwa wa Simba, kwani ni timu bora Afrika, hivyo juu ya Mlima Kilimanjaro ni sehemu sahihi, kwani ni sehemu ya juu zaidi Afrika. Pia tutasaidia jitihada za Serikali kutangaza utalii na Mlima Kilimanjaro," amesela Kajula.
  Simba leo wamezindua huduma tatu, NMB Simba Akaunti, NMB Simba Queens Akaunti na Akaunti ya Watoto ambazo gharama yake ni Shilingi 5000.
  Mapema Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmd Ally alisema kwamba tamasha la Simba Day litafanyika  Agosti 6 badala ya Agosti 8 kama ilivyo kawaida.
  "Simba Day itakuwa Agosti 6, tumeirudisha nyuma siku mbili sababu Agosti 10 tutakuwa na mchezo wa Ngao ya Jamii hivyo tunataka wachezaji wetu wapate muda wa kupumzika," amesema Ahmed Ally.
  Katika shughuli hiyo pia Ally alimtambulisha kwa wanachama, mchezaji mpya mshambuliaji Mcameroon, Leandre Willy Essomba Onana aliyesajiliwa kutoka Rayon Sport ya Rwanda ambaye aliahidi kuisaidia timu kuvuna mataji msimu ujao.
  "Napenda kuushukuru Uongozi wa Simba kwa kunikubali, sitaki kusema mengi lakini nitajitahidi kufanya vizuri ili kuisaidia timu kupata mataji na kufanya timu ijuvunie mimi,” amesema Onana ambaye ni kati ya wachezaji ambao hawajaenda na timu kambini Uturuki kwa sababu tofauti.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: JEZI MPYA ZA SIMBA KUZINDULIWA MLIMA KILIMANJARO IJUMAA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top