• HABARI MPYA

  Alhamisi, Agosti 13, 2020

  SIMBA SC KUTAMBULISHA NEMBO MPYA NA JEZI ZA MSIMU UJAO KUELEKEA SIMBA DAY 2020

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KLABU ya Simba ya Dar es Salaam imebadili nembo yake walioanza kuitumia mwaka 1971 baada ya kubadili jina kutoka Sunderland.
  Hayo yamesemwa leo na Msemaji wa klabu hiyo, Hajji Sunday Manara wakati akizungumza na Waandishi wa Habari katika hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam kueleka Wiki ya Simba 2020 ambayo safari hii itajulikana kama Wiki Ya Mabingwa.
  “Kesho Ijumaa tutazindua nembo mpya ya klabu. Tumeiboresha ili iendane na soko la sasa. Baada ya uzinduzi wa logo mpya tutazindua jezi mpya ya Simba ya msimu. Hii ndio AnotherLevel. Baada ya hapo tunaanza kutangaza na wachezaji wapya,” amesema Manara.
  Amesema kesho baada ya uzinduzi wa nembo mpya na jezi zitakazotumika kwa msimu 2020/2021, pia watazindua rasmi kampeni itakayowapa nafasi mashabiki wa Simba kujishindia jezi pamoja na tiketi kuelekea kilele cha Wiki ya Mabingwa.
  Msemaji huyo ameongeza kwamba Jumamosi kuanzia Saa 2:00 asubuhi watakuwa kwenye ufukwe ya bahari ya Hindi eneo la Daraja la Salender na  Jumapili kuanzia Saa 6:00 mchana watakuwa makao makuu ya klabu kufanya dua. “Kama upo mkoani, fanya kwenye eneo lako,” amesema Manara.
  Aidha, Manara amesema kwamba katika kuiunga mkono Serikali, Jumatatu na Jumanne kupitia matawi yote nchi nzima, wana Simba wote watatembelea vivutio vya utalii hiyo ikiwa ni siku maalumu kuunga mkono utalii wa ndani ya nchi.
  "Pia jumanne kwa kushirikiana na mdhamini mkuu SportPesa tutatoa msaada kwa watoto ambao wanaishi kwenye mazingira magumu na kuwapa jezi. Jumatano, Alhamisi na Ijumaa ni siku za kuchangia damu,”ameongeza Manara.
  Amesema Alhamisi watakwenda Shule ya Uhuru pamoja na wachezaji kuwafariji watoto wenye mahitaji mbalimbali na kuwachangia.
  Amesema Jumatatu wataitaja timu watakayocheza nayo mechi ya kirafiki kwenye kilele cha Wiki ya Simba na viingilio vya mchezo huo. 
  “Kwa mara ya kwanza Simba tutatumia viwanja viwili kwenye tukio moja. Tutatumia Uwanja wa Mkapa na Uwanja wa Uhuru kwa kuweka screen kubwa. Uwanja wa Mkapa peke yake hautoshi,” amesema Manara na kuongeza;
  “Tukio la michezo ambalo linaloongoza nchini ni Simba Day. Mwaka jana tulijaza sana ndio maana mwaka huu tunaomba viwanja viwili. Kilele cha Wiki ya Mabingwa itakuwa jumapili Agosti 23 hapa Serena kufanya sherehe na wageni wetu,”.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC KUTAMBULISHA NEMBO MPYA NA JEZI ZA MSIMU UJAO KUELEKEA SIMBA DAY 2020 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top