• HABARI MPYA

  Tuesday, July 09, 2019

  GARDIEL MICHAEL AWAFUATA KAKOLANYA NA AJIBU SIMBA SC, ASAINI MIAKA MIWILI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  BEKI wa kushoto wa kimataifa wa Tanzania, Gardiel Michael Mbaga amesaini mkataba wa miaka miwili kujiunga na mabingwa wa Bara, Simba SC kutoka kwa mahasimu, Yanga SC.
  Gardiel anajiunga na Simba SC kama mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake na Yanga SC aliyoichezea kwa miaka miwili kufuatia kujiunga nayo kutoka Azam FC iliyomuibua kisoka.
  “Kwa heshima ya ndugu zetu watano wa Azam Media ambao wametutoka tunatangaza usajili muhimu wa eneo la ulinzi, Gardiel Michael, mchezaji wa timu ya Taifa (Taifa Stars) amesaini mkataba wa miaka miwili kuchezea timu yetu ili kuwezesha kuleta makombe na mafanikio zaidi,”imesema taarifa ya Simba SC leo mchana.
  Mtendaji Mkuu wa Simba SC, Crescentius John Magori akimtambulisha Gardiel Michael, mchezaji wa tatu kutoka kwa mahasimu, Yanga  

  Mbaga anakuwa mchezaji mpya wa 10 mpya kusajiliwa Simba SC na wa tatu kutoka Yanga SC baada ya kipa Beno David Kakolanya na kiungo Ibrahim Ajibu Migomba, ambao kwa pamoja na beki wa kati, Kennedy Wilson Juma kutoka Singida United wanafanya idadi ya wachezaji wanne wazawa wapya Msimbazi hadi sasa.
  Wengine sita wote ni wa kigeni, Wabrazil mabeki beki Gerson Fraga Vieira ATK ya Ligi Kuu ya India na Tairone Santos da Silva kutoka klabu ya Atletico Cearense FC, mshambuliaji, Wilker Henrique da Silva kutoka Bragantino, zote za Daraja la Nne nchini Brazil na viungo Mkenya, Francis Kahata Nyambura, Msudan Sharaf Eldin Shiboub Ali Abdalrahman na winga Deo Kanda kutoka TP Mazembe ya kwao, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
  Pamoja na kusaini wachezaji wapya, Simba SC pia imewapa mikataba mipya wachezaji wake kadhaa wa msimu uliopita, wakiwemo kipa Aishi Manula, mabeki Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, Nahodha Msaidizi, Mohammed Hussein ‘Tshabalala, Muivory Coast, Serge Wawa Pascal viungo Jonas Mkude, Mzambia Clatous Chama na washambuliaji Nahodha Mkuu, John Bocco na Meddie Kagere raia wa Rwanda.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: GARDIEL MICHAEL AWAFUATA KAKOLANYA NA AJIBU SIMBA SC, ASAINI MIAKA MIWILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top