• HABARI MPYA

  Jumatatu, Julai 15, 2019

  ALGERIA MA SENEGAL KUKUTANA TENA FAINALI AFCON 2019

  FAINALI ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2019 itazikutanisha timu za Kundi C tupu, Senegal na Algeria Ijumaa wiki hii Uwanja wa Kimataifa wa Cairo nchini Misri.
  Hiyo ni baada ya timu hizo kuibuka na ushindi dhidi ya wapinzani wao, Tunisia na Nigeria katika mechi kali za Nusu Fainali mjini Cairo leo.
  Uwanja wa  Juni 30 mjini Cairo, bao la kujifunga la beki wa AA Gent ya Ubelgiiji, Dylan Bronn dakika ya 100 liliivusha Senegal fainali kwa ushindi wa 1-0.
  Awali, timu zote zilikosa penalti na sifa ziwaendee makipa wote, Alfred Benjamin Gomis wa SPAL ya Italia aliyedaka shuti la kiungo wa Zamelek ya Misri, Ferjani Sassi dakika ya 75 na Mouez Hassen anayedakia Nice II ya Ufaransa aliyepangua mchomo wa kiungo wa Newcastle United, Henri Saivet dakika ya 80.
  Na Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, bao la shuti la mpira wa adhabu la kiungo mshambuliaji wa Manchester City ya England dakika ya 90 na ushei, liliipeleka Algeria fainali baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya Nigeria. 
  Hiyo ni baada ya beki wa Udinese ya Italia, William Troost-Ekong kujifunga dakika ya 40 kuipatia Algeria bao la kuongoza, kabla ya mshambuliaji wa Shanghai Shenhua ya China, Odion Ighalo kuisawazishia Nigeria kwa penalti dakika ya 72.
  Sasa Nigeria itaumana na Tunisia katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu utakaofanyika Jumatano Uwanja wa Al Salam mjini Cairo na fainali itafuatia Uwanja wa Kimataifa wa Cairo Ijumaa.
  Ikumbukwe katika mchezo wa Kundi C, Algeria iliibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Senegal, bao pekee la mshambuliaji wa Esperance ya Tunisia, Mohamed Youcef Belaili dakika ya 49 Uwanja wa Juni 30 mjini Cairo Juni 27.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: ALGERIA MA SENEGAL KUKUTANA TENA FAINALI AFCON 2019 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top