• HABARI MPYA

  Jumanne, Julai 16, 2019

  AZAM FC YAIPIGA TP MAZEMBE 2-1 KIGALI NA KUTINGA NUSU FAINALI KOMBE LA KAGAME

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MABINGWA watetezi, Azam FC wamefanikiwa kwenda Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) leo Uwanja wa Nyamirambo mjini Kigali, Rwanda.
  Haukuwa ushindi mwepesi, kwani Azam FC ililazimika kutoka nyuma ili kupata tiketi ya Nusu Fainali, baada ya kutanguliwa kwa bao la Ipamy Giovanni dakika ya 21.
  Mshambuliaji mpya, Iddi Suleiman ‘Nado’ aliyesajiliwa kutoka Mbeya City alianza kuisawazishia Azam FC dakika ya 27 akimalizia mpira uliorudi baada ya kuokolewa kwa kichwa kufuatia mpira wa adhabu uliopigwa na Mzimbabwe, Bruce Kangwa kutoka kushoto.

  Wachezaji wa Azam FC wakimpongeza Obrey Chirwa baada ya kufunga bao la ushindi wa 2-1 dhidi ya TP Mazembe

  Na alikuwa Iddi Nado mwenyewe aliyesababisha faulo hiyo baada ya kuangushwa na Giovanni pembezoni mwa Uwanja kabla ya beki wa kimataifa wa Zimbabwe kwenda faulo iliyozaa bao lililoirejesha Azam mchezoni.
  Na sifa zimuendee mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa aliyefunga bao la ushindi dakika ya 69 akimalizia krosi ya Abdul Haji ‘Hama Hama’ kutoka upande wa kulia.
  Robo Fainali ya pili inaendelea hivi sasa kati ya KCCA ya Uganda na wenyeji, Rayon Sports wakati nyingine zitafanyika kesho, baina ya wenyeji wengine APR watakaomenyana na Manyema Union na Gor Mahia ya Kenya dhidi ya Green Eagles ya Zambia.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM FC YAIPIGA TP MAZEMBE 2-1 KIGALI NA KUTINGA NUSU FAINALI KOMBE LA KAGAME Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top