• HABARI MPYA

  Wednesday, July 10, 2019

  YANGA SC YAMSAINISHA KIPA NAMBA MBILI WA TAIFA STARS, METACHA BONIPHACE MNATA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KLABU ya Yanga SC imefanikiwa kumsajili kipa namba mbili wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Metacha Boniphace Mnata aliyesaini mkataba wa miaka miwili kutoka Mbao FC ya Mwanza.
  Metacha alikuwa anacheza kwa mkopo Mbao FC kutoka Azam FC, lakini anajiunga na Yanga SC kama mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba na mwajiri wake wa awali.
  Metacha, kama Aishi Salum Manula, kipa namba moja wa Taifa Stars aliibuliwa katika akademi ya Azam kabla ya kuanza kutolewa kwa mkopo ili kupata uzoefu.
  Metacha Mnata (kushoto) akisaini mkataba wa kujiunga na klabu ya Yanga SC  

  Katika misimu hii miwili, Mnata amecheza Mbao FC na Tanzania Prisons na baada ya kumaliza mkataba wake na Azam FC akiwa kwenye mkopo Mwanza, akagoma kuongeza ili kutimiza dhamira ya kujiunga na Yanga.
  Mnata kipa wa zamani wa timu za vijana za U17 na U20 kiu yake ni kuwa mlinda mlango chaguo la kwanza la Taifa Stars na kucheza soka ya kulipwa Ulaya.
  Mnata anakuwa mchezaji mpya wa 14 kusajiliwa na Yanga SC na wa sita tu mzawa, baada ya mabeki Muharami Salum Issa ‘Marcelo’ kutoka Malindi ya kwao, Zanzibar, Ally Mtoni 'Sonso' kutoka Lipuli FC, Ally Ally kutoka KMC ya Kinondoni, viungo wa ulinzi, Abdulaziz Makame kutoka Mafunzo ya Zanzibar na Mapinduzi Balama kutoka Alliance FC ya Mwanza, 
  Wengine saba wote wa kigeni ambao ni kipa Farouk Shikalo kutika Bandari ya kwao, Kenya, Sadney Urikhob kutoka Namibia, Lamine Moro kutoka Ghana, Juma Balinya kutoka Uganda, Issa Bigirimana, Patrick Sibomana wote wa Rwanda, Mustapha Seleman kutoka Burundi na Maybin Kalengo kutoka Zambia.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC YAMSAINISHA KIPA NAMBA MBILI WA TAIFA STARS, METACHA BONIPHACE MNATA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top