• HABARI MPYA

  Saturday, July 20, 2019

  YANGA SC YATAMBULISHA ‘JEZI ZA BARAKA’ ZA MSIMU MPYA ZILIZOING’ARISHA TIMU 1992

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KLABU ya Yanga SC ya Dar es Salaam leo imetambulisha jezi zake za nyumbani za msimu mpya wa 2019-2020 za rangi ya njano na nyeusi za kashata pia, ambazo zinakaribia kufanana na za mwaka 1992 walizopewa nchini Misri.
  Baada ya kutoa sare ya 0-0 na wenyeji, Ismailia mjini Alexandria nchini Misri katika mchezo wa marudiano Hatua ya 32 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika Aprili 4 mwaka 1992, walijitokeza Wazungu waliovutiwa na soka ya Yanga wakawazawadia jezi za rangi ya njano na nyesi za alama ya kashata.
  Pamoja na sare hiyo, Yanga SC ilitolewa kufuatia kufungwa 2-0 katika mchezo wa kwanza Machi 21 mjini Dar es Salaam baada ya awali kuitoa St. Louis ya Shelisheli kwa jumla ya mabao 7-2, ikishinda 3-1 ugenini na 4-1 nyumbani.


  jezi zake za nyumbani za Yanga SC msimu mpya wa 2019-2020 zinakaribia kufanana na za msimu wa 1992-1993 

  Ilipotoka Misri, moja kwa moja ikafikia kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya mahasimu, Simba SC na ikavaa jezi hizo kwa mara ya kwanza na kuibuka na ushindi wa 1-0, bao pekee la Nahodha wake wakati huo, beki wa kushoto Kenneth Pius Mkapa dakika ya 10.
  Ikitumia jezi hizo, Yanga SC ikabeba ubingwa wa Ligi Kuu mwaka 1992 na ikaendelea kutamba hadi 1993 ikiwa na jezi mpya ilipotwaa tena taji hilo pamoja na lile la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati mjini Kampala, Uganda.  
  Bila shaka ni kwa kumbukumbu ya mafanikio hayo, Yanga SC chini ya Mwenyekiti wake mpya, Dk. Mshindo Msolla iomeamua kurudia jezi hizo za bahati kuelekea msimu ujao.
  Yanga iliyoweka kambi mjini Morogoro, itauzindua msimu mpya kwa kumenyana na vigogo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), AS Vita katika mchezo wa kirafiki Agosti 4, Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Mchezo huo utafanyika katika kilele cha Wiki Mwanachi, tamasha maalum la kutambulisha kikosi kipya cha klabu pamoja na jezi za msimu.
  Wachezaji wanaotarajiwa kuchezea Yanga msimu ujao ni makipa; Farouk Shikalo, Metacha Mnata, Ramadhani Kabwili na Klaus Kindoki. 
  Mabeki; Paul Godfrey ‘Boxer’, Juma Abdul, Muharami Issa ‘Marcelo’, Jaffary Mohamed, Andrew Vincent ‘Dante’, Kelvin Yondani, Ally Ally, Mustafa Suleiman, Ally Mtoni ‘Sonso’ na Lamine Moro.
  Viungo; Papy Kabamba Tshishimbi, Said Juma ‘Makapu’, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Mohamed Issa ‘Banka’, Patrick Sibomana, Issa Bigirimana, Mapinduzi Balama, Mrisho Ngassa, Deus Kaseke, Raphael Daud Loth na Abdulaziz Makame ‘Bui’.
  Washambuliaji; Sadney Urikhob, Juma Balinya na Maybin Kalengo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC YATAMBULISHA ‘JEZI ZA BARAKA’ ZA MSIMU MPYA ZILIZOING’ARISHA TIMU 1992 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top