• HABARI MPYA

  Alhamisi, Julai 11, 2019

  AZAM FC YASAJILI MCHEZAJI MPYA KUTOKA IVORY COAST ALIKUWA ANACHEZA GHANA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  UONGOZI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, umekamilisha taratibu za kumsajili kiungo mshambuliaji, Richard Djodi, kwa mkataba wa mwaka mmoja kwa usajili huru akitokea kwa vigogo wa Ghana, Ashanti Gold.
  Huo ni usajili wa mwisho kwa Azam FC kwa ajili ya msimu ujao, ikiwa hadi sasa imesajili wachezaji wapya watano, watatu wakiwa wa kigeni na wawili wazawa.
  Djodi raia wa Ivory Coast, anayemudu kucheza nafasi zote za ushambuliaji, alifanikiwa kufunga jumla ya mabao 17 na pasi 13 za mwisho, katika mechi 35 alizoichezea Ashanti Gold huku katika mechi 12 za mwisho akipiga manne.
  Wachezaji wengine wapya waliosajiliwa na Azam FC chini ya Kocha Mkuu mpya, Mrundi Etienne Ndayiragijje ni Idd Suleiman 'Nado', Suleimani Ndikumana, Emmanuel Mvuyekure na Abalkasim Khamis.

  Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin 'Popat' akibadilishana mikataba na Richard Djodi

   Kwa sasa kikosi cha Azam FC kipo mjini Kigali, Rwanda kinaposhiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame.
  Katika mechi zake mbili za awali za Kundi B, Azam FC imeshinda moja, 1-0 dhidi ya wenyeji, Mukura Victory na kufungwa 1-0 dhidi ya KCCA ya Uganda na kesho itahitimisha mechi zake kundi hilo kwa kumenyana na Bandari ya Kenya Uwanja wa Huye mjini Butare.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM FC YASAJILI MCHEZAJI MPYA KUTOKA IVORY COAST ALIKUWA ANACHEZA GHANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top