• HABARI MPYA

  Jumatano, Julai 24, 2019

  YANGA SC SASA KUMENYANA NA KARIOBANGI SHARKS KATIKA KILELE CHA WIKI YA MWANANCHI

  Na Mwandishi Wetu, MOROGORO
  TIMU ya Yanga SC itamenyana na Kariobangi Sharks ya Kenya Agosti 4, mwaka huu Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam katika kilele cha Wiki ya Mwananchi.
  Hiyo ni baada ya klabu ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kujitoa kwa kubanwa na ratiba ya mechi za awali za Ligi ya Mabingwa Afrika iliyotoka mwishoni mwa wiki.
  Taarifa hii inakuja siku moja baada ya Yanga kushinda mechi ya tatu mfululizo jana katika kambi yake ya Morogoro kujiandaa na msimu upya baada ya kuichapa ATN 7-0 Uwanja wa Chuo cha Biblia, Bigwa mkoani Morogoro.
  Wachezaji wapya wa Yanga, kipa Mkenya Farouk Shikalo (kushoto) na mshambuliaji Mzambia, Maybin Kalengo

  Mshambuliaji wa kimataifa wa Rwanda, Patrick Sibomana alifunga mabao matatu peke yake, huku mengine mawili yakifungwa na nyota wa Namibia, Sadney Urikhob, Mganda Juma Balinya na beki Mghana, Lamine Moro moja kila mmoja.   
  Mechi mbili zilizotangulia Yanga ilishinda 2-0 dhidi ya Moro Kids mabao ya Balinya na beki wa kulia, Paul Godfrey ‘Boxer’ ambaye alikosekana leo kufuatia kujiunga na timu ya taifa ya Tanzania kwa maandalizi ya mchezo wa kufuzu Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) dhidi ya Kenya Jumapili.
  Na mechi ya kwanza Yanga ilishinda 10-0, kiungo mshambuliaji, Mrisho Khalfan Ngassa akifunga mabao matatu peke yake, mengine Feisal Salum, Raphael Daudi, Mapinduzi Balama, Mkongo Papy Kabamba Tshishimbi, Wanyarwanda Patrick Sibomana, Issa Bigirimana na Balinya, 
  Na yote hayo ni maandalizi ya mchezo wao wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga SC wakianza na Township Rollers ya Botswana kati ya Agosti 9 na 11 mjini Dar es Salaam kabla ya kurudiana nao mjini Gaborone kati ya Agosti 23 na 25.
  Ikifanikiwa kuvuka raundi ya kwanza Yanga itakutana na mshindi kati ya Green Mamba ya Eswatini na Zesco ya Zambia.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA SC SASA KUMENYANA NA KARIOBANGI SHARKS KATIKA KILELE CHA WIKI YA MWANANCHI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top