• HABARI MPYA

  Jumatano, Julai 31, 2019

  MSHAMBULIAJI MKONGO AWASILI DAR ES SALAAM KUKAMILISHA USAJILI WAKE YANGA SC

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI David Molinga (pichani kushoto) amewasili Alfajiri ya leo mjini Dar es Salaam kutoka kwao, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa ajili ya kujiunga na klabu ya Yanga.  
  Mchezaji huyo anakuja nchini baada ya kumaliza mkataba na FC Lupopo ya kwao aliyojiunga nayo akitokea Renaissance zote za Ligi Kuu ya RDC, Linafoot.
  Na ujio wa mchezaji huyo unafanya Mkongo mwenzake, kipa Klaus Kindoki aruhusiwe kuondoka klabu hiyo ili Yanga ibaki na wachezaji 10 wa kigeni kwa mujibu wa kanuni.
  Wachezaji wengine wa kigeni Yanga SC ni Nahodha Papy Kabamba Tshishimbi pia kutoka DRC, kipa Mkenya Farouk, Sadney Urikhob kutoka Namibia, Lamine Moro kutoka Ghana, Juma Balinya kutoka Uganda, Issa Bigirimana, Patrick Sibomana wote wa Rwanda, Mustapha Seleman kutoka Burundi na Maybin Kalengo kutoka Zambia.
  Kwa ujumla Yanga SC imeimarisha kikosi chake msimu huu kwa kusajili nyota wengine sita wapya, kipa Metacha Mnata kutoka Mbao FC alikokuwa anacheza kwa mkopo kuoka Azam FC, mabeki Muharami Salum Issa ‘Marcelo’ kutoka Malindi ya kwao, Zanzibar, Ally Mtoni 'Sonso' kutoka Lipuli FC, Ally Ally kutoka KMC ya Kinondoni, viungo wa ulinzi, Abdulaziz Makame kutoka Mafunzo ya Zanzibar na Mapinduzi Balama kutoka Alliance FC ya Mwanza.
  Wakati huo huo, kikosi cha Yanga kinaendelea na mazoezi yake leo mjini Morogoro katika kambi yake ya kujiandaa na msimu mpya baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Friends Rangers jana, mabao ya mshambuliaji wake mpya kutoka Namibia, Sadney Urikhob dakika ya 38 na Nahodha mpya, kiungo Mkongo Papy Kabamba Tshishimbi.
  Yanga SC watamenyana na Kariobangi Sharks ya Kenya Jumapili Uwanja wa taifa mjini Dar es Salaam katika kilele cha Wiki ya Mwananchi.
  Ikiwa kambini mjini Morogoro, Yanga imecheza mechi nne za kujipima nguvu na kushinda zote, 10-1 dhidi ya dhidi ya Tanzanite, 7-0 dhidi ya ATN, 2-0 dhidi ya Moro Kids na 1-0 dhidi ya Mawenzi Market.
  Na yote hayo ni maandalizi ya mchezo wao wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga SC wakianza na Township Rollers ya Botswana kati ya Agosti 9 na 11 mjini Dar es Salaam kabla ya kurudiana nao mjini Gaborone kati ya Agosti 23 na 25.
  Ikifanikiwa kuvuka raundi ya kwanza Yanga itakutana na mshindi kati ya Green Mamba ya Eswatini na Zesco ya Zambia.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MSHAMBULIAJI MKONGO AWASILI DAR ES SALAAM KUKAMILISHA USAJILI WAKE YANGA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top