• HABARI MPYA

  Jumanne, Julai 30, 2019

  CHAMA AFUNGA SIMBA SC YALAZIMISHA SARE YA 1-1 NA ORLANDO PIRATES LEO JO’BURG

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TIMU ya Simba SC imekamilisha mechi zake za kujipima nguvu kwa kulazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na wenyeji, Orlando Pirates katika mchezo wa kirafiki uliofanyika jioni ya leo Uwanja wa Orlando mjini Johannesburg, Afrika Kusini.
  Mabao ya yote ya leo yamefungwa na wachezaji wa kimataifa wa Zambia, akianza Clatous Chota Chama kuifungia Simba SC dakika ya 33, kabla ya mshambuliaji, Augustine Kabaso Mulenga kuisawazishia Orlando Pirates dakika ya 40.
  Huo ulikuwa mchezo wa nne wa kujipima nguvu kwa Simba SC katika kambi yake ya Afrika Kusini kujiandaa na msimu mpya, baada ya awali kushinda mechi mbili mfululizo na kutoa sare moja. 
  Clatous Chama alianza kuifungia Simba SC kabla ya Mzambia mwenzake, Augustine Mulenga kuisawazishia Orlando Pirates 

  Mabingwa hao wa Tanzania Bara walianza kwa kuifunga 4-0 timu ya Chuo Kikuu cha Orbit Tvet, kabla ya kuwachapa wenyeji, Platinums Stars FC 4-1 na kutoa sare ya 1-1 na Township Rollers mechi zote zikipigwa mjini Rusternburg.
  Baada ya mchezo wa leo, Simba itarejea nyumbani kwa ajili ya tamasha la Simba Day Agosti 6 siku ambayo watamenyana na Power Dynamos ya Zambia Uwanja mjini Dar es Salaam katika mchezo mwingine wa kirafiki.
  Simba SC imelazimika kurudisha nyuma kwa siku mbili tamasha hilo ambalo kila mwaka hufanyika Agosti 8 baada ya ratiba ya Ligi Mabingwa Afrika kutoka ikionyesha mechi za kwanza za raundi ya Kwanza zitachezwa kati ya Agosti 9 na 11. 
  Simba SC wataanzia ugenini dhidi ya UD do Songo ya Msumbiji kati ya Agosti 9 na 11 kabla ya kurejea nyumbani kwa mchezo wa marudiano kati ya Agosti 23 na 25.
  Ikifanikiwa kuvuka raundi ya kwanza, Simba itakutana na mshindi kati ya FC Platinum ya Zimbabwe na Nyasa Bullets ya Malawi na ikifuzu mtihani huo pia itaingia tena hatua ya makundi.
  Wakati Simba ni mabingwa wa Bara, Power Dynamos walimaliza nafasi ya sita kwenye Kundi B Ligi Kuu ya Zambia msimu uliopita, ambalo Green Eagles iliongoza na kuingia fainali na kufungwa kwa penalti 3-1 na ZESCO United walioibuka mabingwa wa Zambia baada ya sare ya 0-0.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: CHAMA AFUNGA SIMBA SC YALAZIMISHA SARE YA 1-1 NA ORLANDO PIRATES LEO JO’BURG Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top