• HABARI MPYA

  Thursday, July 11, 2019

  NDAYIRAGIJJE KOCHA MPYA WA TAIFA STARS, WASAIDIZI WAKE NI MGUNDA NA MATOLA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MRUNDI Etienne Ndayiragijje ameteuliwa kuwa kaimu kocha wa Tanzania kwa ajili ya mechi za kuwania tiketi ya Fainali za Ubingwa wa Mataifa wa Afrika (CHAN) mwakani nchini Cameroon.
  Taarifa ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) leo imesema kwamba uamuzi huo umefikiwa kwenye kikao cha dharula cha Kamati ya Utendaji ya bodi hiyo ya soka nchini kilichofanyika jana.
  Aidha, taarifa hiyo imesema kwamba Etienne ambaye ni kocha wa klabu ya Azam FC ya Dar es Salaam, amewapendekeza kocha wa Coastal Union, Juma Mgunda na Kocha Msaidizi wa Polisi Tanzania, Suleiman Matola kuwa wasaidizi wake, Meneja Nadir Haroub 'Cannavaro' na Kocha wa makipa, Saleh Ahmed Machupaa.
  Etienne Ndayiragijje ameteuliwa kuwa kocha wa muda wa Taifa Stars

  Taifa Stars watakuwa wenyeji wa Harambee Stars Julai 27 katika mchezo wa kwanza Raundi ya kwanza ya mchujo wa kuwania fainali za CHAN 2020, michuano inayoshusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee kabla ya timu hizo kurudiana Agosti 2 mjini Nairobi.
  Uteuzi huo unakuja baada ya kufukuzwa kwa kocha Mnigeria, Emmanuel Amunike kufuatia Taifa Stars kupoteza mechi zote tatu za Kundi C kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2019 na taarifa ya TFF imesema uteuzi huo umezingatia programu maalumu ya kuendeleza makocha wazawa. 
  Baada ya kufungwa 2-0 na Senegal, 3-2 na Kenya na 3-0 na Algeria, Taifa Stars iliondoka Misri bila hata pointi moja, ikishika mkia kwenye Kundi C, nyuma ya jirani zao, Kenya waliovuna pointi tatu, huku Senegal iliyomaliza na pointi sita katika nafasi ya pili ikiungana na Algeria iliyokusanya pointi tisa kwenda hatua ya 16 Bora.
  Taifa Stars ya kocha Emmanuel Amunike imeshindwa kuvunja rekodi ya kikosi cha mwaka 1980 kilichoshiriki fainali hizo mjini Lagos, Nigeria ambacho angalau kiliambulia pointi moja baada ya sare na Ivory Coast ya 1-1, kikitoka kufungwa 2-1 na Misri na 3-1 na wenyeji, Nigeria.
  Amunike aliyeng’ara na Super Eagles katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 1994 nchini Marekani akicheza wingi ya kushoto, anaondoka baada ya kuiongoza Taifa Stars katika jumla ya mechi 10, ikishinda mbili tu, kufungwa sita na sare mbili.
  Taifa Stars imekuwa timu ya kwanza ya taifa ya wakubwa Amunike kufundisha, baada ya awali kuwa kocha wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya kwao, Nigeria kuanzia mwaka 2014 hadi 2017.
  Zaidi ya hapo, Amunike mwenye umri wa miaka 47 alifundisha klabu za Al Hazm ya Saudi Arabia, kama Kocha Msaidizi mwaka 2008 kabla ya kuhamia Julius Berger hadi mwaka 2011 alipojiunga na Ocean Boys, zote za Nigeria.
  Alipoachana na U-17 ya Nigeria akaenda kufundisha Al Khartoum SC ya Sudan kuanzia mwaka 2017 hadi 2018 na sasa anakuja kuujaribu ‘mfupa’ uliowashinda wengi, Taifa Stars.   
  Kisoka, Amunike aliibukia klabu ya Concord mwaka 1990 kabla ya kwenda kuchezea Julius Berger 1991, zote za kwao, Nigeria baadaye Zamalek ya Misiri mwaka 1991 hadi 1994 ndipo akahamia Ulaya.
  Alianza na klabu ya Sporting CP ya Ureno kuanzia 1994 hadi 1996 kabla ya kuhamia Barcelona ambako alicheza hadi mwaka 2000 alipohamia Albacete zote za Hispania na mwaka 2003 alijiunga na Busan I'Cons ya Korea Kusini alikocheza hadi 2004 akahamia Al-Wehdat ya Jordan kumalizia soka yake.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NDAYIRAGIJJE KOCHA MPYA WA TAIFA STARS, WASAIDIZI WAKE NI MGUNDA NA MATOLA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top