• HABARI MPYA

  Jumamosi, Julai 20, 2019

  NI ALGERIA MABINGWA AFRIKA, WAIPIGA SENEGAL 1-0 NA KUTWAA TAJI LA PILI AFCON

  BAO la dakika ya kwanza la Baghdad Bounedjah limetosha kuipa Algeria Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Senegal usiku wa Ijumaa Uwanja wa Kimataifa wa Cairo nchini Misri.
  Ushindi huo unazima kiu ya miaka ya 29 ya Algeria ‘Mashujaa wa Jangwani’ kusubiri taji hilo tangu walitwae mwaka 1990 kwa mara ya kwanza nay a mwisho waliposhinda 1-0 pia dhidi ya Nigeria mjini Algiers.
  Mshambuliaji huyo wa Al Sadd ya Qatar, Bounedjah mwenye umri wa miaka 27 aliyechezea Etoile du Sahel ya Tunisa na USM El Harrach ya kwao, Algeria awali alifunga bao lake akimalizia kazi nzuri ya beki kinda wa miaka 21 wa Empoli ya Italia, Ismael Bennacer.

  Wachezaji wa Algeria wakimnyanyua kocha wao, Djamel Belmadiin baada ya ushindi wa AFCON 

  Bao hilo liliakumbusha Simba wa Teranga machungu ya mwaka 2002 walipofungwa na Cameroon kwenye fainali kwa penalti 3-2 baada ya sare ya 0-0 mjini Bamako nchini Mali.

  Senegal walilalamika kunyimwa penalti kipindi cha pili baada ya Djamel Benlamri kuonekana ameushika mpira kwenye boksi uliopigwa na Sarr kutoka upande wa kulia, lakini refa Neant Alioum wa Cameroon pamoja na awali kutenga tuta, lakini akabadili uamuzi wake kufuatia kutazama marudio ya picha za video (VAR).
  Ikumbukwe Jumatano Nigeria ‘Super Eagles’ ilifanikiwa kumaliza nafasi ya tatu baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Tunisia, bao pekee la mshambuliaji wa Shanghai Shenhua ya China, Odion Jude Ighalo dakika ya tatu.
  Wenyeji, Misri na mabingwa watetezi, Cameroon wote safari yao iliishia hatua ya 16 Bora, Mafarao wakichapwa 1-0 na Afrika Kusini ‘Bafana Bafana’ na Simba Wasiofungika wakipigwa 3-2 na Nigeria.
  Zote Algeria na Senegal zimetoka Kundi C ambako zilikuwa na timu kutoka Mashariki mwa Afrika, Kenya na Tanzania waliokuwa wakishiriki kwa mara ya pili tu fainali hizo baada ya mwaka 1980 Nigeria.  
  Kikosi cha Algeria kilikuwa; M’Bolhi, Zeffane, Mandi, Benlamri, Bensebaini; Guedioura, Bennacer, Feghouli/Tahrat dk85, Mahrez, Bounedjah/Slimani dk88 na Belaili/Brahimi dk84.
  Senegal; Gomis, Gassama, Sane, Kouyate, Sabaly, Ndiaye/Diatta dk59, Gueye, Saivet/Diagne dk75, Sarr, Mane na Niang/Keita dk85.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: NI ALGERIA MABINGWA AFRIKA, WAIPIGA SENEGAL 1-0 NA KUTWAA TAJI LA PILI AFCON Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top