• HABARI MPYA

  Jumanne, Julai 09, 2019

  IVORY COAST, TUNISIA ZAKAMILISHA ROBO FAINALI AFCON 2019

  TIMU za Ivory Coast na Tunisia zimefanikiwa kutinga Robo Fanali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) baada ya kuzitoa Ghana na Mali katika mechi za jana nchini Misri.
  Ivory Coast ilikuwa ya kwanza kutinga hatua ya Nane Bora ya AFCON baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Mali, bao pekee la Wilfried Zaha dakika ya 76 Uwanja wa New Suez akimalizia pasi ya mshambuliaji mwenzake, Jonathan Kodjia wa Aston Villa, zote za England. 
  Tunisia ikafuatia kuing’oa Ghana kwa penalti 5-4 kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 120 Uwanja wa Ismailia. 
  Mshambuliaji wa Esperance, Taha Yassine Khenissi alianza kuifungia Tunisia dakika ya 73 akimalizia pasi ya kiungo Wajdi Kechrida, kabla ya Rami Bedoui anayecheza naye wa Etoile du Sahel zote za nyumbani, Tunisia kujifunga dakika ya 90 na ushei kuisawazishia Ghana.  Bao pekee la Wilfried Zaha limeipeleka Ivory Coast Robo Fainali AFCON 2019

  Katika mikwaju ya penalti waliofunga upande wa Tunisia ni Naim Sliti wa Dijon, Wahbi Khazri za Ufaransa, Dylan Bronn wa Gent ya Ubelgiji, Yassine Meriah wa Olympiakos Piraeus ya Ugiriki na Ferjani Sassi wa Zamalek ya Misri.
  Na waliofunga penalti za Ghana ni Mubarak Wakaso wa Alaves ya Hispania, Jordan Ayew anayehamia Swansea City kutoka Crystal Palace, Lumor Agbenyenu wa Goztepe ya Uturuki na Thomas Teye Partey wa Atletico Madrid ya Hispania wakati Caleb Ekuban wa Trabzonspor ya Uturuki pekee ndiye aliyekosa.      
  Ivory Coast na Tunisia zimeungana na Senegal, Benin, Nigeria, Afrika Kusini, Algeria na Madagascar kutinga hatua ya Robo Fainali ya AFCON 2019, michuano ambayo imeshuhudiwa bingwa mtetezi, Cameroon na mwenyeji, Misri wakiishia hatua ya 16 Bora.
  Robo fainali za kwanza zitachezwa kesho, Senegal na Benin Saa 1:00 usiku Uwanja wa Juni 30 na Nigeria na Afrika Kusini Saa 4:00 usiku Uwanja wa Kimataifa wa Cairo na za mwisho zitachezwa Alhamisi kati ya Ivory Coast na Algeria Saa 1:00 usiku Uwanja wa New Suez na Madagascar na Tunisia Saa 4:00 usiku Uwanja wa Al Salam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: IVORY COAST, TUNISIA ZAKAMILISHA ROBO FAINALI AFCON 2019 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top