• HABARI MPYA

  Jumamosi, Julai 20, 2019

  KAGERA SUGAR YAICHAPA AIGLE NOIR FC YA BURUNDI 3-0 MCHEZO WA KIRAFIKI CHAMAZI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TIMU ya Kagera Sugar ya Bukoba leo imeibuka na ushindi wa 3-0 dhidi ya Aigle Noir FC ya Burundi katika mchezo wa kirafiki wa kujiandaa na msimu mpya uliofanyika Uwanja wa Azam Complex mjini Dar es Salaam.
  Mabao ya Kagera Sugar yamefungwa na viungo Peter Mwalyanzi dakika ya 47, Yussuf Mhilu dakika ya 64 na mshambuliaji Evarigestus Mujwahuki dakika ya 90 na ushei. 
  Baada ya kupepesuka msimu uliopita na kukaribia kuteremka daraja, Kagera Sugar imejidhatiti kuhakikisha hairudii makosa msimu huu na tayari imeanza maandalizi.
  Kagera Sugar ilianza kwa kusajili jumla ya wachezaji 11 wapya wakiwemo wawili wa kigeni, Mganda Jackson Kibirige kutoka Bakavu Dawa FC ya Jamhuri ya Kodemokrasia ya Kongo (DRC) na Moussa Hadji Mosi kutoka Leslierres ya Ligi Kuu ya kwao, Burundi.

  Wengine wote ni wazawa kipa Benedicto Tinocco kutoka Mtibwa Sugar ya Morogoro, Abdul Swamadu Kassim kutoka Malindi FC ya Zanzibar, Yussuph Mhilu kutoka Yanga SC aliyecheza kwa mkopo Ndanda FC msimu uliopita, Zawadi Mauya kutoka Lipuli FC, Ally Shomari kutoka Mtibwa Sugar, Abdallah Seseme kutoka Mwadui FC, Awesu Ally Awesu kutoka Singida United, Erick Kyaruzi, Frank Ikobela, wote kutoka Mbeya City ya Mbeya na  Evarist Mjwahuki kutoka Mbao FC ya Mwanza.
  Ikumbukwe Kagera Sugar na Mwadui FC zilinusurika kushuka daraja baada ya kubaki Ligi Kuu ya Tanzania Bara kupitia mechi zao Play-Off dhidi ya Pamba SC na Geita Gold Mine za Daraja la Kwanza. 
  Mabao ya Ally Ramadhani dakika ya 51 na Japhet Makalayi dakika ya 59 yaliipa Kagera Sugar ushindi wa 2-0 dhidi ya Pamba SC Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba Juni 9 baada ya timu hizo kutoka sare ya kwenye mchezo wa kwanza Juni 3 Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza.
  Na hiyo ni baada ya Kagera Sugar kumaliza nafasi ya 18 katika Ligi Kuu, nyuma ya Mwadui FC iliyomaliza nafasi ya 17 ambayo iliitoa Geita Gold katika mechi ya mchujo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KAGERA SUGAR YAICHAPA AIGLE NOIR FC YA BURUNDI 3-0 MCHEZO WA KIRAFIKI CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top