• HABARI MPYA

  Jumapili, Julai 21, 2019

  AZAM FC YASHINDWA KUTWAA TENA KOMBE LA KAGAME, YAPIGWA 1-0 NA KCCA KIGALI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TIMU ya KCCA ya Uganda imefanikiwa kutwaa taji la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Azam FC ya Dar es Salaam Uwanja wa Nyamirambo mjini Kigali leo.
  Bao lililoipa ushindi huo Timu ya Mamlaka ya Jiji la Kampala limefungwa na Mustafa Kiiza dakika ya 62 aliyemtungua kipa Mghana wa Azam FC, Razack Abalora kwa shuti la mguu wa kushoto. 
  Kwa ushindi huo, KCCA wamezawadiwa dola za Kimarekani 30,000, huku washindi wa pili, Azam FC wakipewa kifuta jasho cha dola 20,000 na washindi wa tatu, Green Eagles ya Zambia dola 10,000.

  Nahodha wa Azam FC, Mzimbabwe Bruce Kangwa akikabidhiwa mfano wa hundi ya dola 20,000 baada ya kufungwa na KCCA leo katika fainali

  Ushindi huo unamaanisha KCCA wanatwaa taji lao la pili tu la kombe la Kagame kihistoria baada ya awali kulitwaa mwaka 1978 ilipoifunga Simba ya Tanzania pia katika fainali.
  Aidha, kwa ushindi huo KCCA wameendeleza ubabe wao kwa Azam FC baada ya kuilaza 1-0 pia Julai 9 katika mchezo wa Kundi B na kumaliza kileleni wakifuatiwa na timu hiyo ya Tanzania.
  Azam FC walikuwa wakilishikilia taji hilo tangu mwaka 2015 baada ya kulitwaa mara mbili mfululizo nyumbani, Dar es Salaam 2015 wakiifunga Gor Mahia ya Kenya 2-0 na 2018 walipoichapa Simba 2-1, mechi zote zikipigwa Uwanja wa Taifa.
  Azam FC imeshindwa kuwa timu nyingine ya Tanzania, baada ya Yanga SC kutwaa Kombe la Kagame nje ya ardhi ya nyumbani. Yanga SC ilibeba taji hilo mara mbili nje ya nyumbani, mwaka 1993 na 1999 mjini Kampala, Uganda.
  Azam waliiingia fainali baada ya ushindi wa penalti 5-4 Ijumaa kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 120 dhidi ya AS Manyema Union ya DRC hapo hapo Uwanja wa Nyamirambo, wakati KCCA iliifunga Green Eagles ya Zambia 4-3 katika mchezo uliodumu kwa dakika 120 baada ya sare ya 2-2 ndani ya dakika 90
  Mapema jioni ya leo Green Eagles ilifanikiwa kumaliza nafasi ya tatu baada ya kuichapa Manyema Union 2-0, mabao ya Edward Mwamba dakika ya 28 na Amity Shamende dakika ya 69 Uwanja wa Nyamirambo pia.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM FC YASHINDWA KUTWAA TENA KOMBE LA KAGAME, YAPIGWA 1-0 NA KCCA KIGALI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top