• HABARI MPYA

  Jumapili, Julai 21, 2019

  SAMATTA AISAIDIA GENK KUTWAA TAJI LA SUPER CUP YA UBELGIJI, YAIPIGA MECHELEN 3-0

  Na Mwandishi Wetu, GENK 
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta  jana ameisaidia klabu yake, KRC Genk kutwaa Super Cup ya Ubelgiji baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya KV Mechelen Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk.
  Huo ulikuwa ni mchezo wa kuunganisha mataji baina ya mabingwa wa Ligi, KRC Genk dhidi ya washindi wa Kombe KV Mechelen kuashiria ufunguzi wa msimu mpya nchini humo.
  Na mabao ya Genk yalifungwa na beki mwenye umri wa miaka 28, Sebastien Dewaest dakika ya 14 na 60 na mshambuliaji kinda wa umri wa miaka 21, Dante Vanzeir la tatu dakika ya 83, wote Wabelgiji.
  Mbwana Samatta akifurahia na taji la Super Cup ya Ubelgiji baada ya kuiwezesha Genk kushinda 3-0 dhidi ya KV Mechelen  
  Mbwana Samatta akifurahia wenzake taji la Super Cup ya Ubelgiji baada ya ushindi wa 3-0 dhidi ya KV Mechelen  
  Mbwana Samatta akiondoka na mpira katikati ya wachezaji wa KV Mechelen 

  Samatta alicheza kwa dakika 71 tu mchezo huo wa kwanza kwake wa msimu kabla ya kumpisha Vanzeir aliyekwenda kuhitimisha ushindi wa Genk kwa kufunga bao la tatu.
  Genk inacheza mechi nyingine leo, itakapoteremka Uwanja wa Het Kuipje kumenyana na wenyeji Westerlo katika mchezo wa kirafiki kabla ya Ijumaa ijayo kucheza mechi yake yake ya kwanza ya msimu mpya wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji dhidi ya Kortrijk Uwanja wa Luminus Arena.
  Ikumbukwe Samatta msimu uliopita aliisaidia KRC Genk kutwaa taji la Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji huku naye akimaliza nafasi ya pili kwa ufungaji wa mabao. 
  Kwa ujumla, Samatta mwenye umri wa miaka 26, ameichezea Genk mechi 156 za mashindano yote na kuifungia mabao 62 tangu amejiunga nayo Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
  Katika ligi ya Ubelgiji pekee amefunga mabao 47 katika mechi 122, kwenye Kombe la Ubelgiji amefunga mabao mawili katika mechi tisa, Super Cup mechi moja na Europa League amefunga mabao 14 katika mechi 24.
  Kikosi cha KRC Genk kilikuwa; Vukovic, De Norre, Cuesta, Dewaest, Uronen, Berge, Heynen, Piotrowski/Nygren dk63, Ito/Ndongala dk76, Benson na Samatta/Vanzeir dk71. 
  KV Mechelen: Verrips, Van Cleemput, Bijker, Swinkels, Togui, Storm/Bosiers dk80, Van Damme/Vranckx dk89, Schoofs, Engvall/De Camargo dk66, Corryn na Peyre.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SAMATTA AISAIDIA GENK KUTWAA TAJI LA SUPER CUP YA UBELGIJI, YAIPIGA MECHELEN 3-0 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top