• HABARI MPYA

  Ijumaa, Julai 12, 2019

  AZAM FC YATINGA ROBO FAINALI KOMBE LA KAGAME, KAZI IMEBAKI KWA KMC KESHO

  Na Mwandishi Wetu, KIGALI
  TIMU ya Azam FC imefanikiwa kwenda Robo Fainali ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame pamoja na kulazimishwa sare ya 0-0 na Bandari ya Kenya katika mchezo wa mwisho wa Kundi B leo Uwanja wa Huye mjini Butare.
  Sare hiyo inaifanya Azam FC inayofundishwa na kocha Mrundi, Etienne Ndayiragijje imaliza na pointi nne kufuatia kushinda 1-0 dhidi ya Mukura Victory na kufungwa 1-0 na KCCA katika mechi zake mbili za awali.
  Mechi nyingine ya kundi hilo leo, KCCA iliibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya wenyeji, Mukura Victory hapo hapo Uwanja wa Huye. 
  Mabao ya KCCA yalifungwa Mike Mutyaba dakika ya tano na Allan Okello dakika ya 42, wakati la Mukura Victory lilifungwa na Gael Duhayindavyi.

  Mshambuliaji wa Azam FC, Obrey Chirwa (kushoto) akimpita mchezaji wa Bandari leo mjini Kigali

  Azam FC imefanikiwa kwenda Robo Fainali ya michuano ya Kombe la Kagame 

  Sasa KCCA inamaliza na pointi saba kileleni mwa kundi ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi nne, wakati Bandari iliyomaliza na pointi tatu ni ya tatu na Mukura yenye pointi moja imeshika mkia.
  Michuano hiyo itaendelea kesho kwa mechi za mwisho za Kundi A; Atlabara ya Sudan Kusini dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kuanzia Saa 10:30 jioni na wenyeji wengine, Rayon Sports dhidi ya wawakilkishi wengine wa Tanzania, KMC ya Dar es Salaam kuanzia Saa 1:00 usiku Uwanja wa Nyamirambo mjini Kigali.
  Jumapili zitahitimishwa mechi za Kundi D kwa Gor Mahia ya Kenya kumenyana na KMKM ya Zanzibar kuanzia Saa 8:00 mchana kabla ya Port ya Djibouti kukipiga na Manyema Union ya DRC kuanzia Saa 10: 30 jioni.
  Tayari Kundi C limekamilisha mechi zake kwa wenyeji wengine APR kuongoza kwa pointi zake tisa, wakifuatiwa na Green Eagles ya Zambia waliomaliza na pointi sita na wote wanakwenda Robo Fainali wakizipiku Prolin ya Uganda iliyomaliza na pointi tatu na Heegan ya Somalia iliyotoka mikono mitupu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM FC YATINGA ROBO FAINALI KOMBE LA KAGAME, KAZI IMEBAKI KWA KMC KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top